Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MZEE WA FACT: Vikwazo vitatu kwa Fei Toto kutua Yanga

Mfungaji bora na MVP wa msimu uliopita, Stephane Aziz Ki, ameondoka Yanga na kuwaacha na kazi ngumu ya kuziba pengo lake.

Majina kadhaa yamependekezwa lakini hakuna jina linalotajwa mara nyingi na kujirudia rudia kwenye vikao vyao kama la Feisal Salum,

maarufu kama Fei Toto, Failasufi au Zanzibar Finest.

Yanga wanamtaka Feisal Salum kwa sababu zote duniani za kimpira, za kibiashara, na hata za kisiasa.


Sababu za kimpira

Fei Toto ni mchezaji mzuri sana ambaye kuwa naye kwenye timu yako ni faida kubwa sana kiufundi kwa sababu anakupa namba na sanaa ya mpira.

Kwenye namba anakupa mabao na pasi za usaidizi wa mabao. Kwenye sanaa

ya mpira anakupa ladha, yaani udambwi na vikolombwezo vya kulifanya jukwaa likaange chipsi.

Yanga wanahitaji vitu hivi kwa msimu ujao ambao wanataka kufanya vizuri kimataifa, ili kuziba kelele za Simba.


Sababu za kibiashara

Yanga wana mpango wa kugoma kwenda kucheza na Simba Juni 15 kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara. Ikitokea hivyo maana yake watakatwa alama 15 na kupoteza ubingwa ambao hatima yake ipo mikononi mwao wenyewe.

Japo wanaweza wakajidanganya kuwa ni ushujaa kufanya hivyo sasa,

lakini akili zao zitakapowarudia, watagundua kwamba walifanya ujinga.

Hii itawatafuna sana na lazima watatafuta kitu cha kujipozea ili kuwasahaulisha mashabiki wao na hakuna kitu kizuri kama Feisal


Salum kwa wakati huo.

Kama Yanga wataupoteza ubingwa kwa misimamo yao isiyo na tija, basi ni

lazima wawe na kitu fulani mkononi cha kutamba nacho kwenye Siku ya

Mwananchi ili kujipoza ndipo linaporudi jina la Feisal Salum.

Pia kumekuwa na tetesi nyingi sana na za muda mrefu kwa Feisal Salum kuhitajika Simba, wapinzani wao wakuu.

Endapo watampata watakuwa wamefunga bao la kisigino na kujiongezea haki ya kutamba mbele ya Simba.


Sababu za kibiashara

Kurudi kwa Fei Toto Yanga kutawafanya wauze jezi nyingi kuelekea msimu mpya na kurahisisha kazi ya kulitangaza Tamasha la Siku ya Mwananchi.

Jezi za Feisal zitauzwa kama njugu na mahudhurio ya siku ya mwananchi


yatakuwa juu sana.

Jina la Fei Toto ni kubwa sana na Yanga wanaamini mchezaji mkubwa kama

huyo anapaswa kuchezea timu yao ili kuongeza thamani ya mechi zao kwenye viingilio na matangazo ya biashara kutoka kwa wadhamini.

Sababu hizi tatu zinalifanya jina la Feisal Salum litawale vichwa vya wafanya maamuzi wa Yanga na kujikuta wakifanya kila jitihada


kuhakikisha wanampata.

Hata hivyo, kuna vikwazo vikubwa vitatu vinavyokwamisha mipango yao hadi sasa.


1. Fei Toto mwenyewe

Feisal Salum alijiunga na Yanga mwaka 2018 akitolewa kama zawadi na mmoja wa mashabiki wao kindakindaki ambaye wakati

huo alikuwa akimiliki timu ya Singida United iliyomsajili kutoka JKU ya Zanzibar.

Akasaini mkataba wa miaka miwili na mwaka 2020 akasaini mkataba mpya wa miaka minne, uliotakiwa kumalizika mwaka 2024.

Lakini akiwa katikati ya mkataba huu, yaani mwaka 2022, Yanga wakaanza

kufanya kufuru kwa kumwaga fedha na kuleta vyuma, akiwemo Aziz Ki.

Wachezaji hawa walilipwa pesa nyingi sana, kuanzia za kusaini mikataba hadi mishahara na posho zingine.

Fei Toto kuona hivyo, akataka na yeye aboreshewe maslahi yake lakini

uongozi wa Yanga chini ya Mhandisi Hersi Said ukampuuza na kusema asubiri hadi mkataba wake uishe.

Aziz Ki alipofika akapangiwa nyumba ya kifahari ya kuishi, lakini siku

chache nyuma yake, Feisal Salum aliomba klabu imuongee shilingi laki

tatu tu kwenye kodi ya nyumba yake maeneo ya Kijitonyama, klabu ikakataa.

Akijiangalia mshahara aliokuwa akilipwa wa shilingi milioni nne kwa mwezi, huku mchezaji mpya (Aziz Ki) akilipwa shilingi milioni 23, akaumia moyo.

Jitihada zake za kutaka aongezewe maslahi zilipogonga mwamba, akaamua


kuununua mkataba wake ili awe huru.

Akawalipa hela zao zilizotajwa na mkataba endapo atataka kuuvunja, Yanga wakakataa, huo ndio mwanzo wa ugomvi wa Fei Toto na Yanga.


Vita ikawa kubwa, kesi ikapelekwa TFF lakini

haikusikilizwa akapeleka shauri kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS).

Lakini kabla haijaanza kusikilizwa, Rais Samia Suluhu Hassan akawasihi Yanga wamalizane naye wakakubali na Fei akawa huru.

Namna alivyopuuzwa alipotaka aboreshewe maslahi wakati ule bado inamjia akilini na anawaona Yanga kama watu fulani hivi wasio na utu ndani yao, kwamba wanajifanya wema kwa sasa ili wampate kujisafisha mbele ya watu hataki kurudi!


2. Rais Samia

Maombi ya Mama Samia kwa Yanga kumalizana na Feisal Salum, hayakuja

hivi hivi. Feisal Salum na timu yake ya utetezi ilipeleka maombi kwa mama awasaidie kumalizana na Yanga.

Walitoa sababu nyingi za kwanini Feisal Salum hataki kuendelea kuitumikia klabu hiyo, lakini kubwa kuliko zote ni manyanyaso.

Walisema Yanga ilimnyanyasa sana katika kipindi chote alichokaa pale

na bado wanaendelea kumnyanyasa kwa kukataa kumuachia huru licha ya kutekeleza matakwa ya kimkataba.


Ndipo mama alipowaomba Yanga wamalizane naye, ile siku ya sherehe aliyowaandalia kuwapongeza kufika Fainali ya Kombe la Shirikisho.

Feisal na kambi yake wanaona haitokuwa heshima kwa mheshimiwa Rais, endapo atarudi kwenye timu waliyosema inawanyanyasa.

Wataonekana waongo na baadaye huko mbele watakosa pa kukimbilia yakiwakuta ya kuwakuta.


3. Mama mzazi wa Fei Toto

Wakati wa sakata la Feisal Salum kuondoka Yanga, mama yake alifanya mahojiano na moja ya vyombo vya habari na kusema mwanaye amekuwa akiteseka sana akiwa Yanga kiasi cha kula ugali na sukari.

Kauli hii iliwakera Wanayanga na kuanza kumshambulia mama huyo bila

staha. Miongoni mwa watu waliosikika kumshambulia mama huyo ni pamoja na afisa habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe.

Mama wa watu kaweka kinyongo mambo yote yale na hataki kabisa kusikia mwanaye anarudi Yanga.

Kwa hiyo licha ya jitihada kubwa ambazo Yanga wanaendelea kuzifanya,

lakini wajue kwamba kinachowakwamisha hadi sasa ni hivi vitu vitatu.

Ni hadi watakapopata suluhu ya vitu hivi ndipo watakapofanikiwa kumrudisha kundini Fei.

Na muda unaenda kasi sana wakati wao wanahangaika kupata suluhu ya mambo haya, Azam FC wenyewe wapo kwenye harakati za kumuongezea mkataba na wengine kama Kaizer Chiefs wapo kwenye harakati za kuboresha ofa yao. Kazi kwao Yanga!