Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwamnyeto ameshinda vita ya maisha

HAKUNA atakayeshtuka akiambiwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Stephane Azizi KI ametoa asisti mbili katika mchezo wa timu yake wala hakuna atakayeshtuka akiambiwa beki wa kulia wa Yanga, Djuma Shaban ametengeneza krosi mbili za mabao.
Wapo watakaoshtuka wakisikia beki wa kati wa Yanga, Bakari Nondo Mwamnyeto ametoa asisti mbili za mabao akitokea eneo lake la ulinzi, hiki ndicho kinachowafanya wengi kujiuliza juu ya ubora wa nahodha huyu kwasasa.
Kuna mabadiliko makubwa yanapita kwa Mwamnyeto ambaye ni miezi michache nyuma alikuwa anaonekana kama sio mtu muafaka tena kwa Yanga na zikaanza hata hesabu za kuanza kutafuta beki mpya wa kati.
Hatua ya Mwamnyeto kuanza kusemwa vibaya zilianza pale msimu uliopita baada ya mechi ya Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), kufuatia timu yake kuruhusu mabao matatu wakitoa sare ya mabao 3-3 dhidi ya Coastal Union wakidai beki huyo alifanya makosa makubwa kisha kila Yanga iliporuhusu bao lawama nyingi zilikuwa kwa beki huyo.


MAKOCHA WALISIMAMA NAYE
Kitu kikubwa ambacho kilimfanya Mwamnyeto kupitia kipindi kigumu ndani ya Yanga ni kutokana na kukabiliwa na matatizo binafsi na hatua ya kwanza ilikuwa pale alipofiwa na mkewe Januari 8, 2021 kutokana na changamoto ya uzazi.
Hizi hazikuwa taarifa ambazo zingemfanya beki huyo wa zamani wa Coastal Union kurudi katika utulivu wake kwa haraka ilimtingisha lakini kabla hajawa sawa sawa akapata changamoto za kuuguliwa na baba yake mzazi Mzee Nondo.
Wakati wote wa matatizo haya ukiacha msiba uliomkuta, mengine alikuwa akipambana nayo ndani kwa ndani na watu wenye msaada kwake walikuwa makocha wake Nasreddine Nabi na hata wasaidizi wake Cedric Kaze na Helmy Gueldich ambao kwa mara kadhaa walikuwa wakipambana kumweka sawa kisaikolojia.
Haya yote yalimuondoa kwenye kiwango chake lakini bahati mbaya mashabiki waliopo nje hawakuwa wanajua wakiona kila Yanga iliporuhusu bao basi beki huyo amekuwa njia ya wapinzani.
Ukiacha makocha wake kumuamini hata viongozi wa klabu hiyo pia walimuamini na kuamua kumpa mkataba mwingine mpya wa kuendelea kusalia ndani ya klabu hiyo wakiamini kwamba mambo anayokabiliana nayo yatapita.


ALIZIBA MASIKIO, AKAPAMBANA
Wakati wote wa kulaumiwa sana hakutaka kuzingatia yanayozungumzwa nje ya uwanja, vuta picha lawama alizokuwa akipewa mitandaoni lakini hata pale alipokuwa uwanjani presha kubwa ilikuwa juu yake.
Nyakati zote hizi ngumu alijua kuishi kama mchezaji mkubwa anavyotakiwa kuishi pengine na wale ambao alikuwa anakuwa nao karibu kwenye timu yake, hakuyumba aliendelea kujipanga na hasa kutumia nafasi vuzuri kila alipokuwa anapewa muda wa kucheza akitokea benchi mpaka wakati huu ambao nafasi yake imerudi kwenye kikosi cha kwanza.


KIWANGO KITU CHA MUDA
Kuna msemo wa Kiingereza unasema 'form is temporary class is permanent' (Kiwango kitu cha muda lakini daraja ni la kudumu), msemo huu unatufundisha kujua kuwavumilia wachezaji na hata klabu zetu kwa wakati mwingine.
Mwamnyeto ni binadamu anaweza kuwa na wakati mbaya kazini kwake lakini hilo ni suala la muda haliwezi kuishi hapo kwake milele, baada ya kuyumba kwa kiwango chake sasa amerudi uwanjani akiwa yule Mwamnyeto wa miaka minne nyuma.
Wote waliokuwa wanamuona kama ni beki aliyefikia mwisho sasa watakuwa wanaona aibu kwa kinachoendelea kwa beki huyu, beki mwenye mwili kama Mwamnyeto taratibu wanazidi kupotea katika kizazi chetu na bahati mbaya tukaanza kucheza karata mbaya kupambana kumpoteza zaidi kwa kumuona amekwisha, hili linaweza kutukumbusha kuwavumilia wachezaji kwamba kuna wakati wanapitia nyakati ngumu pia.


ANAUPIGA MWINGI
Mwamnyeto sasa amerudi katika ubora wake hakuna anayemsema vibaya tena zaidi anaendelea kutushangaza na kutucheka tuliokuwa tunamuandama kwa lawama mbalimbali, anafanya kazi kubwa kwenye ukuta wa timu yake akiwa kiongozi wa mfano uwanjani anakaba, anawakumbusha wenzake kama kiongozi lakini anakuwa saehemu ya kuanzisha mashambulizi kama ambavyo anahitajika kufanya beki yoyote wa kisasa.
Mchezo wa ugenini dhidi ya Rivers United ya Nigeria beki huyo anafanya kitu 'nondo' kwa kupiga asisti mbili matata kwa mshambuliaji wake Fiston Mayele na hazikuwa asisti za kuungaunga bali ni zile za kiwango cha kidunia ambazo zikaenda kutengeneza ushindi mkubwa kwa timu yake.


AMEIONGEZEA KITU TIMU
Kurejea kwa kiwango cha Mwamnyeto kuna faida kwa timu yake na hata wachezaji wenzake, siku zote timu bora ni ile inayotengeneza ushindani wa nafasi ya wachezaji wake katika kila namba.
Ukiangalia kikosi cha Yanga sasa kina mabeki wa kati watatu waliokatika kiwango bora Mwamnyeto, Dickson Job na pia Ibrahim Abdullah 'Bacca', uwepo wa mabeki hawa watatu bora unawaimarisha wote kiushindani na kila mmoja kuhakikisha anakuwa katika kiwango bora ili asipoteze nafasi.
Utamu zaidi ni makocha wao ambao nao kama sio kuchagua wawili wamekuwa na matumizi nao hata wote watatu kutumika kwa pamoja na bado Yanga ikafanya vizuri kwa kupata matokeo pia lango lao kuwa salama kama ambavyo ilitokea katika mchezo wa ugenini dhidi ya Rivers.


HUYU HAPA NABI

Akizungumza nyakati ngumu alizokutana nazo kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema wao waliamini bado Mwamnyeto ni mchezaji mzuri licha ya kupitia kipindi kifupi cha mpito akikabiliwa na mambo mbalimbali,.

"Changamoto hazikuwa tu kwa Mwamnyeto wako wachezaji wengi wanakutana na hicho kipindi hakuna maana kwamba wameisha kiwango lakini huwa tunakaa nao na kuwapa moyo na wakati mwingine kuwasaidia kutoka katika nyakati ngumu," alisema Nabi.

"Kwasasa ameanza kurudi katika kiwango chake kila mtu anamuona sasa ameimarika, hata sisi sote kwenye timu tuna furaha kuona amerudi kwa nguvu, wachezaji wakubwa wengi wanakuwa na ujasiri wa namna hii kwa kuzipita nyakati ngumu, aliweka juhudi pia yeye mwenyewe kwa kumsikiliza kila mmoja aliyekuwa akimshauri vizuri huku ndani."