Mwakinyo kavunja ukimya

Muktasari:
- Mwakinyo aliyewahi kuingia kwenye 20 bora ya dunia kwenye uzani wa super welter na namba moja nchini kwenye kila uzani ‘pound for pound’ ameporomoka kote na sasa ni wa pili nchini na wa 66 duniani.
BAADA ya kuwa kimya ulingoni tangu mwaka jana alipochapwa kwa TKO na Liam Smith nchini Uingereza, bondia Hassan Mwakinyo amefunguka kila kitu na kueleza mipango yake ijayo.
Mwakinyo aliyewahi kuingia kwenye 20 bora ya dunia kwenye uzani wa super welter na namba moja nchini kwenye kila uzani ‘pound for pound’ ameporomoka kote na sasa ni wa pili nchini na wa 66 duniani.
“Yote ni kwa sababu sijacheza muda mrefu, lakini siku si nyingi nitarudi kwenye nafasi yangu,” alisema Mwakinyo juzi alipozungumza na Mwanaspoti.
Bondia huyo mwenye nyota tatu alisema Aprili mwaka huu mashabiki wake watamwona tena ulingoni mjini Dodoma.
“Nitacheza Dodoma na bondia kutoka nje ya nchi, naamini litakuwa ni pambano langu bora na kubwa litakalonirudisha kwenye renki. “Naendelea na mazoezi, niko fiti na naamini pambano hilo litanirudisha kwenye ubora,” alisema.
Katikati ya mwaka jana, Mwakinyo alianza kuporomoka polepole hata baada ya pambano na Smith alilopoteza kwa Technical Knock Out (TKO) aliendelea kuporomoka mpaka sasa, matokeo hayo yakichangizwa na kutocheza muda mrefu.