Chelsea kuchagua yenyewe Ulaya

Muktasari:
- Chelsea itacheza fainali ya Conference League dhidi ya Real Betis huko Wroclaw, Poland, Mei 28, mwaka huu.
LONDON, ENGLAND. NDO hivyo. Chelsea italazimika kuchagua inataka kucheza michuano gani msimu ujao, Ligi ya Mabingwa Ulaya au Europa League.
The Blues itakuwa na fursa hiyo ya wingi wa machaguo endapo itashinda ubingwa wa Europa Conference League na kisha ikafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kumaliza ndani ya nafasi tano za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Kwenye fainali ya Conference League, kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Enzo Maresca kitakabiliana na Real Betis huko Wroclaw, Poland, Mei 28.
Mshindi wa Conference League sambamba na kupata kombe na zawadi ya Pauni 5.9 milioni, itanyakua pia tiketi ya kucheza michuano ya Europa League kwa msimu unaofuatia.
Lakini, mambo yanaweza kuiacha njiapanda kama itafuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kupitia tiketi ya nafasi kwenye ligi ya ndani. Kama Chelsea inayopewa nafasi kubwa ya kushinda Wroclaw na huku ikiwa imemaliza ndani ya Top Five kwenye Ligi Kuu England, kanuni inairuhusu kuchagua kama inataka kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya au Europa League.
Ni kitu kisichotarajiwa kwa klabu kama Chelsea kuchagua kucheza kwenye michuano mingine kuliko la Ligi ya Mabingwa Ulaya na kufuzu tu michuano hiyo kuna mkwanja wa Pauni 70 milioni mezani.
Hata hivyo, kinachoelezwa ni kanuni hiyo ya kuchagua michuano iliwekwa kwa timu ndogo kwa timu za Ulaya ambazo zitakuwa zimeshinda ubingwa wa Conference League.
Chelsea kwa sasa inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na imebakiza mechi mbili za kupambania kuwamo ndani ya Top Five ili kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao na mechi zilizobaki ni Manchester United na Nottingham Forest.