Chelsea kumaliza kazi Conference League

Muktasari:
- Mchezo wa fainali ya Conference League utafanyika Mei 28 mwaka huu nchini Poland kwenye Uwanja wa Wrocław ambapo mshindi wa jumla baina ya Chelsea au Djurgaarden atakutana na mshindi wa jumla baina ya Real Betis au Fiorentina.
London, England. Chelsea itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Stamford Bridge kuikabili Djurgårdens kutoka Sweden katika mchezo wa marudiano wa nusu fainali ya UEFA Conference League, ikiwa na faida kubwa ya ushindi wa mabao 4-1 ilioupata katika mchezo wa kwanza uliofanyika kwenye Uwanja wa 3Arena, Stockholm, Sweden.

Katika mchezo huo uliochezwa jijini Stockholm, Chelsea ilionyesha ubora wa hali ya juu, hasa katika safu ya ushambuliaji iliyosababisha mabao kupitia kwa Nicolas Jackson aliyefunga mara mbili, Jadon Sancho na Noni Madueke. Bao la kufutia machozi kwa upande wa Djurgården lilifungwa kupitia mpira wa kona kipindi cha pili.

Kocha wa Chelsea, Enzo Maresca amesema wamejipanga kufanya vizuri katika mchezo wa marudiano kwani wanaamini mchezo bado haujamalizika.
“Tuna faida ya kuwa mbele kwa mabao 4-1, lakini tuna kumbukumbu ya mchezo dhidi ya Legia Warsaw, ambapo tulishinda 3-0 ugenini lakini tukapata wakati mgumu kwenye mechi ya nyumbani, hivyo tunahitaji kuwa makini kwenye mechi ya leo," amesema kocha wa Chelsea, Enzo Maresca.

Djurgården wanakabiliwa na msimu mgumu. Licha ya kufika hatua hii ya nusu fainali kwa mara ya kwanza, timu hiyo ya Sweden imekuwa na mwenendo wa kusuasua ndani ya ligi ya nyumbani ikiwa imepata ushindi mara moja katika mechi saba zilizopita huku ikikabiliwa pia na majeruhi kwa wachezaji wake jambo linawafanya kupewa nafasi ndogo ya ushindi dhidi ya Chelsea.

Mchezo mwingine wa nusu fainali utafanyika kule Italia kwenye Uwanja wa Artemio Franchi ambapo Fiorentina itakuwa nyumbani kuikabili Real Betis huku mchezo ukionekana bado mgumu kwani timu zote zina nafasi ya kusonga fainali licha ya Betis kuwa mbele kwa maba 2-1 iliyoyapata kwenye mchezo wa kwanza.

Fiorentina ambayo inanolewa na kocha, Raffaele Palladino, inapambana kufika katika fainali ya tatu mfululizo ya michuano hii, licha ya kupoteza fainali mbili zilizopita dhidi ya West Ham (2022/23) na Olympiacos (2023/24). Katika mchezo wa kwanza, Fiorentina ilipata bao la kufutia machozi kupitia kwa kiungo Rolando Mandragora, lakini ilishindwa kuzuia ushindi wa Betis uliopatikana kwa mabao ya Isco na Antony.
Katika mchezo wa leo, Fiorentina inatarajiwa kuanza na safu ya ushambuliaji inayoongozwa na Moise Kean na Albert Gudmundsson, huku David De Gea akisimama langoni wakati kwa upande wa Real Betis itaongozwa na washambuliaji kama Cedric Bakambu, Isco na Antony.

Mchezo wa fainali ya Conference League utafanyika Mei 28 mwaka huu nchini Poland kwenye Uwanja wa Wrocław ambapo mshindi wa jumla baina ya Chelsea au Djurgaarden atakutana na mshindi wa jumla baina ya Real Betis au Fiorentina.