Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mukwala apiga tatu, Simba ikiichapa Coastal

Muktasari:

  • Simba inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 54 na Coastal Union ipo nafasi ya tisa ikiwa na pointi 24.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Simba, Steven Mukwala leo amegeuka shujaa wa timu hiyo baada ya kuifungia mabao yote matatu (hat trick) katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Kwa kufunga ‘hat trick’ hiyo, Mukwala anakuwa mchezaji wa kwanza wa Simba kufanya hivyo katika Ligi Kuu msimu huu huku akiwa wa tatu baada ya nyota wawili wa Yanga, Prince Dube na Stephane Aziz Ki ambao ndio walitangulia kufunga mabao matatu katika mchezo mmoja kwa nyakati tofauti.

Nyota ya Mukwala katika mchezo huo ambao ulitawaliwa na Simba kwa muda mrefu, imeanza kung’aa katika dakika ya 30, alipofunga bao la kwanza baada ya kuunganisha kwa shuti la mguu wa kulia, pasi ya David Kameta.

Katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza, Mukwala tena aliihakikishia Simba uongozi katika mchezo huo baada ya kuifungia bao la pili akimalizia pasi ya Elie Mpanzu na hivyo Simba kwenda mapumziko ikiwa inaongoza kwa mabao 2-0.

Dakika 11 tu baada ya kipindi cha pili kuanza, Mukwala aliifungia Simba bao la tatu ambalo ni la nane kwake kwenye Ligi Kuu msimu huu baada ya kumalizia kwa shuti kali mpira uliotemwa na kipa Chuma Ramadhan baada ya shuti la Mpanzu.

Katika mchezo huo, Simba imefanya mabadiliko ya kuwatoa Charles Ahoua, Yusuph Kagoma, Mpanzu, Kibu Denis na Mukwala ambao nafasi zao zilichukuliwa na Awesu Awesu, Fabrice Ngoma, Joshua Mutale, Leonel Ateba na Ladack Chasambi.

Coastal Union yenyewe imewatoa Lucas Kikoti, Maulid Shaban na Gustaph Saimon ambao nafasi zao zilichukuliwa na Enrick Nkosi, Bakari Selemani na Mbaraka Yusuph.

Ushindi huo umeifanya Simba kujichimbia katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ambapo imefikisha pointi 54, nne nyuma ya Yanga ambayo inaongoza ikiwa na pointi 58.

Coastal Union kwa kupoteza mechi ya leo imeendelea kubakia katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 24.

Matokeo ya leo kwa upande mwingine yameifanya Simba kuendeleza ubabe ugenini kwenye Ligi Kuu msimu huu ambapo katika mechi 11 ilizocheza hadi sasa, imeshinda kumi na kutoka sare moja.

Coastal Union inafikisha mechi ya tano mfululizo kwenye Ligi Kuu bila kupata ushindi ikitoka sare tatu na kupoteza michezo miwili.