Prime
Kisa Yanga, Che Malone awaumiza vichwa Simba

Muktasari:
- Che Malone raia wa Cameroon, amekuwa ndiye mhimili wa safu ya ulinzi akishirikiana na Abdulrazak Hamza msimu huu na kuifanya iwe timu iliyoruhusu mabao machache.
Dar es Salaam. Simba inatarajiwa kushuka uwanjani leo jioni kuikabili Coastal Union, lakini akili za benchi la ufundi na mabosi wa klabu hiyo kwa sasa ni Dabi ya Kariakoo itakayopigwa Machi 8 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini kuna mshtuko walioupata kupitia beki wa kati tegemeo, Fondo Che Malone.
Beki huyo raia wa Cameroon, amekuwa ndiye mhimili wa safu ya ulinzi akishirikiana na Abdulrazak Hamza ana wakati mwingine Chamou Karaboue waliotua msimu huu na kuifanya iwe timu iliyoruhusu mabao machache hadi sasa katika Ligi Kuu Bara, ikifungwa manane tu katika mechi 20.
Katika kuhakikisha beki wa kati wa Simba, Fondoh Che Malone anarudi mapema uwanjani baada ya kuwa majeruhi, mabosi wa klabu hiyo wamemtafutia daktari maalum ili amsaidie apone haraka jeraha alilonalo, hesabu zikiwa katika Dabi ya Kariakoo itakayopigwa wikiendi ijayo jijini Dar es Salaam.
Beki huyo Mcameroon anayeitumikia Simba kwa msimu wa pili sasa, aliumia siku ya pambano la Dabi ya Mzizima dhidi ya Azam FC na kutolewa dakika chache tangu kuanza kwa pambano hilo lililooisha kwa sare ya mabao 2-2.
Ukuta wa Simba umekuwa ukimtegemea Che Malone akishirikiana na mabeki wengine wawili, akiwamo mzawa Abdulrazak Hamza na Chamou Karaboue raia wa Ivory Coast na kuifanya timu hiyo kuwa na ukuta wa zege ulioruhusu mabao machache (manane) kuliko timu zote kwa sasa katika Ligi Kuu Bara.
Simba iliyopo jijini Arusha kwa sasa kwa ajili ya pambano la leo la Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union, inajua ikimalizana na Wagosi itakuwa na kibarua kingine kizito mbele ya watani wao wa jadi, Yanga Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa na deni la kipigo cha 1-0 ilichopewa katika mchezo wa kwanza uliopigwa Oktoba 19, mwaka jana.
Presha inayoikimbiza Simba ni inapata wasiwasi juu ya kumkosa Che Malone katika mchezo dhidi ya Yanga kutokana na majeraha hayo aliyoyapata na hivyo ili kuona anapona haraka, klabu imeamua kumtafuta daktari maalumu wa kumsaidia wakati timu ikiwa Arusha na imembakisha jijini Dar es Salaam.
Nyota mwingine atakayekosa mechi ya leo ni kipa Moussa Camara aliyetibuliwa na majeraha baada ya kucheza mechi zote 20 za Ligi Kuu akiwa na kikosi hicho.
Hesabu za Simba ziko hivi, wameangalia mabeki wake waliosalia akiwemo Chamou Karaboue na Hussein Kazi mmoja wao anaweza kuziba nafasi ya Che Malone kwenye mchezo dhidi ya Coastal Union, lakini wanapata wasiwasi kuikabili Yanga, ambayo imekuwa na rekodi nzuri ya kufunga mabao kupitia nyota wenye kasi, Clement Mzize, Prince Dube, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz KI.
Simba ina uhakika wa kuwatumia Hamza na Chamou kwenye mchezo wa leo dhidi ya Coastal Union, lakini presha yao ni washambuliaji wa Yanga ambao wanaona wana kasi kuliko beki huyo raia wa Ivory Coast ambaye anaonekana kukosa kasi, tofauti na ilivyo kwa Hamza na Malone.
"Tunapambana Che Malone awe sawasawa haraka kama itawezekana, ndiyo maana unaona hajaonekana mazoezini, kuna daktari maalum amepatiwa ili ahakikishe anawahi mechi ya watani," alisema bosi wa juu wa klabu hiyo aliyekataa kutajwa gazetini aliyeongeza;
"Wale washambuliaji wa Yanga wanatakiwa kudhibitiwa na mabeki wenye uzoefu mkubwa kama Che Malone, hawa wengine tunapata wasiwasi sana, hata hivyo bado tuna mabeki wengine wa kati wanaoweza kufanya kazi kwa ufanisi kulingana na kocha Fadlu Davids atakavyotaka."
Katika mechi iliyopita ya Dabi ya Kariakoo, Yanga ilishinda bao 1-0 lililotokana na beki wa Simba, Kelvin Kijili kujifunga katika harakati za kuokoa mpira na kufanya Wekundu kutimiza mechi nne mfululizo mbele ya watani wao bila kupata ushindi.