Mtazamo tofauti kifungo cha Mwakinyo

Dar es Salaam. Licha ya Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) kutangaza kumfungia bondia Hassan Mwakinyo kwa mwaka mmoja, wabobezi wa masuala ya ngumi nchini wamesema kifungo hicho kitamuathiri bondia huyo nchini, lakini kimataifa bado ana uwezo wa kupigana.
Hata hivyo, rais wa TPBRC, Chaurembo Palasa aliliambia gazeti hili jana jioni kwamba kama bondia huyo atatumia ujanja wa kutumia kibali cha nchi nyingine kucheza kimataifa atakuwa amekiuka kanuni na hatua zaidi dhidi yake zitachukuliwa na kamisheni hiyo.
Jana Katibu Mkuu wa TPBRC, George Silasi alitangaza kufungiwa kwa bondia huyo na kutozwa faini ya Sh1 milioni kwa kile alichodai ni kujichukulia uamuzi bila kuheshimu mkataba kwenye pambano lake na Julius Indongo, Septemba 29, mwaka huu ambalo Mwakinyo aligoma kupigana kwa kile alichodai promota alikiuka mkataba.
Baada ya vuta nikuvute ya pande zote, TPBRC iliomba vielelezo vya pande zote mbili, kabla ya jana kutoa uamuzi wa kumfungia Mwakinyo kuzichapa ndani na nje ya nchi kwa mwaka mmoja na kutakiwa kulipa faini ya Sh1 milioni haraka.
Mmoja wa wadau wa ngumi ambaye hakupenda jina lake kuandikwa gazetini, alisema adhabu hiyo itamuathiri Mwakinyo hapa nchini na siyo kimataifa kama ataamua kutumia leseni ya nchi nyingine.
Akitoa mfano wa bondia Harrison Nii Lartey wa Ghana aliyewahi kufungiwa nchini mwake na TPBRC kumpa leseni ya Tanzania kwenda kuzichapa nchini Russia na Abdulkerim Edilov 2021, bondia huyo wa zamani aliyewahi kuongoza ngumi nchini alisema adhabu hiyo itamuathiri Mwakinyo kwa mapambano ya Tanzania, lakini kimataifa haina mashiko yoyote.
“Anaweza kutumia leseni ya nchi nyingine na akacheza bila wasiwasi. Hizi ni ngumi za kulipwa ni kama biashara. Utafungiwa huku unakwenda kucheza kwingine. Hapa nchini adhabu itamuathiri ukizingatia hata mapromota wa hapa wengi ni kama wamemchoka, lakini akipata pambano kimataifa akaamua kucheza anaweza kwa kutumia leseni ya nchi nyingine na TPBRC haitafanya chochote,” alisema kiongozi huyo wa zamani wa ngumi.
Hata hivyo aliyewahi kuwa promota wa Mwakinyo, Ally Mwazoa alisema adhabu hiyo itamuathiri bondia huyo kama Kamisheni itaamua kumuongezea kwa kukiuka taratibu.
“Kucheza kimataifa wakati wowote anaweza kwa kutumia kibali cha nchi nyingine, lakini kamisheni kwa hapa nchini ndiyo imeshikilia mpini. Akifanya hivyo inaweza kumkomoa kwa kumpa adhabu zaidi ya hiyo kwa hapa Tanzania. Ni vyema akawa mpole tu,” alisema.
Kwa upande wake, Chaurembo Palasa alisema ili Mwakinyo acheze kipindi hiki cha adhabu ni kuhama nchini, akifanya hivyo haitamzuia, lakini kama atatumia ujanja huo watamsubiri atakaporudi adhabu itaendelea.