Msuva hashikiki kwa mabao Ligi Kuu Iraq

Muktasari:
- Saimon Msuva alijiunga na Al Talaba, Agosti 2024 akitokea Al Najma ya Ligi Daraja la Kwanza Saudi Arabia.
Bao moja ambalo Saimon Msuva ameifungia timu yake ya Al Talaba dhidi ya Al Karma juzi kwenye Ligi Kuu ya Iraq, limemfanya nyota huyo wa Taifa Stars kufikisha mabao tisa kwenye ligi hiyo, idadi ambayo inamfanya abakize mabao matano ili avunje rekodi yake aliyojiwekea msimu wa 2018/2019.
Rekodi ambayo Msuva anaiwinda ni ya kufunga idadi kubwa ya mabao ndani ya msimu mmoja tangu alipoanza kucheza soka la kulipwa ambapo hadi sasa, mabao 13 aliyofunga katika Ligi Kuu ya Morocco akiwa na Difaa El Jadida bado haijafikiwa.
Msuva ambaye aliwahi kuitumikia Yanga kisha kujiunga na Difaa El Jadida ya Morocco, msimu wa kwanza kwenye Ligi hiyo alipachika mabao 11 katika mechi 10 na msimu uliofuata akaivunja kwa kufunga mabao 13 katika michezo 28.

Mwaka 2020 akajiunga na Wydad Casablanca ambayo katika msimu wa 2020/2021 aliifungia mabao saba katika mechi 27 na msimu uliofuata katika mechi tisa alipachika mabao matatu tu.
Baada ya kuachana na Wydad, msimu wa 2022/2023 Al Qadisiya iliyokuwa ligi daraja la kwanza Saudi Arabia ambayo katika mechi nane aliifungia mabao nane na baada ya msimu huo kumalizika alijiunga na JS Kabylie ya Algeria ambayo hakuifungia bao lolote katika mechi nane alizoichezea msimu wa 2023/2024.
Msimu uliopita, aliichezea Al Najma ya Ligi Daraja la Kwanza Saudi Arabia ambapo katika mechi tatu alifunga mabao manne na msimu huu akajiunga na Al Talaba aliyoifungia mabao tisa katika mechi nane.
Katika kudhihirisha kuwa Msuva hajabahatisha kufunga mabao hayo, mshambuliaji huyo ameyafunga katika mechi nane mfululizo ambapo katika michezo saba alifunga bao mojamoja na mabao mawili alipachika katika mchezo mmoja.
Al Talaba anayochezea Msuva, inashika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu ya Iraq ikiwa na pointi 44 na imebakiza mechi moja dhidi ya Al Kahraba.
Mshauri wa benchi la ufundi la Taifa Stars, Jamhuri Kihwelo 'Julio' alisema kuwa Msuva anachokifanya sio kigeni kutokana na juhudi na nidhamu yake.
"Msuva ni mchezaji mwenye heshima na nidhamu na amekuwa anacheza kwa kujitolea ndio maana amekuwa akifanya vizuri katika kila timu anayocheza," alisema Julio.