Prime
Msimu bora na rekodi kwa Yanga

Muktasari:
- Yanga imemaliza msimu na pointi 82, ikishinda mechi 27, sare moja na kupoteza miwili kati ya 30 iliyocheza, ikitwaa taji la 31, la Ligi Kuu tangu mwaka 1965, huku Simba ikiwa ya pili na pointi 78, ikishinda 25, sare tatu na kupoteza miwili.
Dar es Salaam. Yanga imetetea tena taji la Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Simba katika mechi ya 'Kariakoo Derby' iliyopigwa juzi, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ikiwa ni rekodi kwao kati ya misimu minne ya ubingwa mfululizo.
Mechi hiyo ya mwisho iliamua bingwa wa Ligi Kuu msimu huu kutokana na tofauti ya gepu la pointi moja kabla ya kukutana ambapo Yanga ilihitaji sare au ushindi tu kwa sababu ilikuwa inaongoza na pointi 79, nyuma ya Simba iliyokuwa na pointi 78.
Katika mechi hiyo ya juzi, Pacome Zouzoua aliifungia Yanga bao la kwanza kwa penalti ya dakika ya 66 baada ya nyota huyo kufanyiwa madhambi eneo la hatari na kipa wa Simba, Moussa Camara, huku Clement Mzize akifunga pia la pili dakika ya 86.
Yanga imemaliza msimu na pointi 82, ikishinda mechi 27, sare moja na kupoteza miwili kati ya 30 iliyocheza, ikitwaa taji la 31, la Ligi Kuu tangu mwaka 1965, huku Simba ikiwa ya pili na pointi 78, ikishinda 25, sare tatu na kupoteza miwili.
Taji hilo ni la 31 kwa jumla tangu mwaka 1965, ila ni la nne mfululizo kwa Yanga kuanzia msimu wa 2021-2022, 2022-2023, 2023-2024 na 2024-2025, ikijibu mapigo kwa Simba iliyochukua pia msimu wa 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021.
Katika misimu hiyo yote minne ambayo Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, msimu huu ndio umekuwa bora zaidi tofauti na iliyopita, kutokana na idadi kubwa ya mabao ambayo kikosi hicho imeyafunga, sambamba na kukusanya pointi nyingi pia.
Msimu wa 2021/2022
Msimu wa 2021-2022, chini ya Kocha, Mtunisia Nasreddine Nabi, Yanga ilimaliza kinara na pointi zake 74, baada ya kushinda mechi 22 na kutoka sare minane, huku ikiwa haijapoteza wowote, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 49 tu na kuruhusu manane.
Kwa upande wa wapinzani wao wakubwa hapa nchini Simba, msimu huo wa 2021-2022, ilimaliza nafasi ya pili na pointi zake 61, baada ya kushinda mechi 17, sare 10 na kupoteza tatu, ambapo safu ya ushambuliaji ilifunga mabao 41 na kuruhusu 14.
Msimu huu pamoja na Yanga kutopoteza lakini, ilifungwa mabao machache kuliko kipindi kingine chote cha misimu minne.
Msimu wa 2022/2023
Msimu wa 2022-2023, Yanga ikifundishwa tena na Nabi, ilitetea taji hilo baada ya kumaliza na pointi 78, baada ya kushinda mechi 25, ikitoka sare tatu na kupoteza mbili, ikifunga mabao 61 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 18, hiki ni kipindi ambacho pamoja na Yanga kutwaa ubingwa lakini timu hiyo iliruhusu mabao mengi.
Msimu huo, Simba ilimaliza nafasi ya pili baada ya kukusanya pointi 73, ikizidiwa tano zaidi, ikishinda mechi 22, sare saba na kupoteza moja, ambapo safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ilifunga mabao 75 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 17.
Baada ya Nabi kuipa Yanga ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili mfululizo huku akiweka rekodi mbalimbali za ndani na nje kwa maana ya kimataifa, akaondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Kocha, Miguel Gamondi raia wa Argentina aliyeipa ubingwa pia.
Msimu wa 2023/2024
Gamondi aliipa Yanga ubingwa msimu wa 2023-2024, baada ya kuiongoza timu hiyo kushinda mechi 26, ikitoka sare miwili na kupoteza pia miwili kati ya 30 iliyocheza, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 71 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 14.
Msimu huo, Simba ilimaliza nafasi ya tatu ikiwa na pointi 69 sawa na Azam FC iliyomaliza ya pili ila zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa tu, ambapo kikosi hicho cha Msimbazi kilishinda mechi 21, sare sita na kupoteza mitatu ndiyo msimu ambao Ynaga ilitoa ubingwa kwa gepu dogo la pointi.
Safu ya ushambuliaji ya Simba ilifunga mabao 59 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 25, jambo lililoifanya kuzidiwa na Azam iliyomaliza ya pili kwa tofauti ya mabao, baada ya timu hiyo kufunga 63, na kuruhusu 21, ikiwa ni zaidi ya manane.
Msimu wa kihistoria
Msimu huu sasa, ndio wa kihistoria zaidi baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mbele ya watani zao wa jadi Simba, kufuatia kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Huu umekuwa msimu bora zaidi kwa kukusanya pointi ambapo wamekusanya pointi 82, ambapo timu hiyo imefungwa mabao 10 tu, lakini imefunga pia idadi kubwa ya mabao baada ya kupachika 83 ambayo ni mengi kuliko misimu yote minne
Hamdi na rekodi ya Omog
Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi ameandika rekodi nyingine mpya ya kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho, huku akiingia katikati ya msimu, akifuata pia nyayo za aliyekuwa Kocha wa Azam FC raia wa Cameroon, Joseph Marius Omog.
Hamdi mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa huku akiwa na leseni A ya UEFA, alitua nchini kujiunga na Singida Black Stars, Desemba 30, 2024, ingawa hakuiongoza hata mechi yoyote hadi Yanga ilipoinasa saini yake rasmi, Februari 4, 2025.
Kocha huyo, alitambulishwa Yanga baada ya kuondoka kwa Mjerumani, Sead Ramovic aliyejiuzulu mwenyewe, Februari 4, 2025, kwa makubaliano ya pande mbili, tangu atambulishwe kikosini humo Novemba 15, 2024, akitokea TS Galaxy ya Afrika Kusini.
Baada ya kuondoka Ramovic aliyejiunga na CR Belouizdad ya Algeria, ndipo Hamdi akakiongoza kikosi hicho na kukipa taji la nne mfululizo la Ligi Kuu Bara na la 31, kwa ujumla tangu mwaka 1965, akiwa ameingia pia katikati ya msimu huu tu.
Katika Ligi Kuu Bara, mechi hiyo na Simba ilikuwa ya 13 kwa Hamdi kuiongoza Yanga tangu alipoanza kibarua hicho Februari 4, 2025, ambapo ameshinda 12 na kutoka suluhu mmoja tu ambao ilikuwa ya kwanza dhidi ya JKT Tanzania, Februari 10, 2025.
Mechi hiyo ya suluhu (0-0), dhidi ya maafande wa JKT Tanzania iliyopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni, ndio iliyokuwa ya kwanza kwa kocha huyo, japo kuanzia hapo ameshinda zote 12, mfululizo hadi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu.
Sasa kitendo cha Hamdi kutwaa ubingwa huo, kinakumbushia msimu wa 2013-2014, ambao Azam FC ilitwaa pia taji la Ligi Kuu, ambapo ilianza msimu na Kocha raia wa England, Stewart Hall, kisha kuondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Joseph Omog.
Hall alitua nchini akiwa kocha wa timu ya taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes' kwa ajili ya kurithi mikoba ya Souleman Sane, ambaye ni baba mzazi wa nyota wa timu ya taifa ya Ujerumani na klabu ya Bayern Munich ya Ujerumani, Leroy Sane.
Kocha huyo alitua Azam FC msimu wa 2010-2012, ingawa aliondoka Novemba 7, 2013, baada tu ya mechi ya mwisho ya mzunguko wa kwanza msimu wa 2013-2014, dhidi ya Mbeya City ya jijini Mbeya, iliyofanyika Azam Complex na kuisha sare ya mabao 3-3.
Yanga yatibua rekodi Simba
Kitendo cha Simba kupoteza pambano la mwisho kwa mabao 2-0, sio kuendeleza tu unyonge kwa Yanga katika Ligi Kuu Bara, kwani pia rekodi ya timu hiyo ya kucheza mechi nyingi bila ya kupoteza imevunjwa, tangu mara ya mwisho ilipochapwa, Oktoba 19, 2024.
Tangu Simba ilipochapwa bao 1-0, dhidi ya Yanga, Oktoba 19, 2024, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, kikosi hicho kilikuwa kimecheza jumla ya mechi 23, bila ya kupoteza, ambapo kati ya hizo kilishinda 21, huku miwili iliyobaki ikimalizika kwa sare.
Kitendo cha Yanga kushinda tena, kimeifanya kuivurugia Simba kwani tangu pambano hilo la Oktoba 19, 2024, liliipa nguvu ya kucheza mechi 23, bila ya kupoteza, kabla ya rekodi hiyo kuja kutibuliwa Juni 25, 2025, ilipokubali kuchapwa mabao 2-0.
Mechi 20 bila kupoteza
Wakati Yanga ikisherehekea ubingwa huo, ila imeendeleza pia rekodi bora ya kutopoteza mechi ya Ligi Kuu, kwani kikosi hicho tangu mara ya mwisho kichapwe mabao 3-1, dhidi ya Tabora United, Novemba 7, 2024, hakijapoteza hadi msimu unaisha.
Tangu Novemba 7, 2024, Yanga imecheza mechi 20 za Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza, ambapo kati ya hiyo imeshinda 19, huku mmoja ukiisha suluhu (0-0) dhidi ya JKT Tanzania, uliopigwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Februari 10, 2025.
Msikie kocha Yanga
Baada ya mechi hiyo, Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi anasema imekuwa furaha kubwa kwake kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho kwa mara ya kwanza, huku akiwapongeza viongozi na mashabiki kwa sapoti waliyompatia tangu mwanzo.
"Kwangu ni heshima kubwa sana lakini hizi zote ziende kwa wachezaji kwa kutambua malengo ya timu yalikuwa ni nini kiasi cha kufanikisha hili, bado tuna taji moja lililobaki ambalo pia tunahitaji kuchukua ili tumalize vizuri msimu," anasema.
Kocha huyo alisema sababu nyingine iliyochangia Yanga kutwaa ubingwa ni kutokana na ubora wa wachezaji wa kikosi hicho, licha ya kukiri ugumu wa kutoa nafasi ya kucheza kwa sababu ya ushindani wa namba uliopo baina ya mchezaji na mchezaji.