Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Msigwa awaita CAF wakague uwanja wa Benjamin Mkapa

Dodoma. Baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kutoa tangazo la kuufungia Uwanja wa Michezo wa Benjamin Mkapa, Serikali imesema walitakiwa kuwasiliana nao kabla ya kuufungia kwa sababu ulishakarabatiwa.

Akizungumza leo Machi 12,2025, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,Gerson  Msigwa amethibitisha kupokelewa kwa tangazo la kuufungia uwanja huo leo asubuhi.

“Ni kweli leo wameamka na hiyo taarifa kuwa CAF wameufunga uwanja wa Benjamin Mkapa kwa sababu za dosari katika eneo la kuchezea. Ukaguzi wa CAF ulifanyika kama wiki mbili zilizopita na ulifanyika baada ya mechi ya Simba na Azam na kumbukeni sisi uwanja tulishautangaza kuufunga kupisha ukarabati,”amesema.

“Lakini hizi mechi zinakuwa na mashabiki wengi na mambo mengi ya kiusalama. TFF (Shirikisho la mpira wa Miguu Tanzania) likatuomba tunaomba tutumie uwanja, siku wamekuja pale uwanja ulikuwa umekatwa nyasi hadi chini kabisa. Kwa hiyo wachezaji walipokuwa wanacheza na unajua hizi mechi zina presha kidogo ukaenda unachimbika chimbika kidogo,”amesema.

Msigwa ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, amesema wakati wanacheza mchezo huo, wakaguzi wa CAF walikuwepo na waliwaeleza kuwa wahakikishe wanarekebisha na wakataka kuona mashine za kurekebishia sehemu ya kuchezea (pitch).

Hata hivyo, amesema hawakuweza kuwaonyesha kwa kuwa mashine hizo zilikuwa njiani zinatoka kwa mtengenezaji nchini China.

Msigwa amesema mashine hizo ziliingia nchini baada ya siku tano tangu walipotaka kuziona na kutumika kufanya ukarabati wa uwanja huo.

“Hata ‘derby’ (la Simba na Yanga) kama ingefanyika juzi Benjamin Mkapa uko tayari. Baada ya tangazo lao la asubuhi tumewasiliana na TFF tukawaambia waambieni waje wakague leo uwanja,”amesema.

“Huwezi kukagua wiki mbili zilizopita halafu unakuja kuufunga uwanja baada ya wiki tatu, leo uwanja uko tayari mashine zimekuja, uwanja umeshakarabatiwa na uko tayari,”amesema Msigwa.

Amesema walitangaza uwanja unakarabatiwa na kuwa hizo mechi wanazofanya kwenye uwanja huo ni kwa maombi yao.

Amesema wao (Serikali) hawakutaka mechi zifanyike pale kwa sababu ni lazima kumwacha  mkandarasi akarabati hadi amalize.

“Kwa sisi kuendelea kutumia uwanja wakati unakarabatiwa unatuongezea gharama. Huu uwanja ulitakiwa kukamilika Agosti (2024) yaani hadi leo haujakamilika mmenielewa. Waje kuangalia uwanja umeshakarabatiwa na lile tangazo walitakiwa kutuambia kabla ya kulitoa,”amesema.