Morocco ana heshima yake apewe
Muktasari:
- Hata alipoanza kucheza mpira ukubwani, jina likamng'ang'ania na akaendelea nalo, hadi likavuka bahari na kufika Zanzibar kwa Hemed Suleiman.
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, chini ya kocha mzawa, Hemed Suleiman 'Morocco' imetoka sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Jamhuri ya Kongo au Kongo Brazzaville, Septemba 5, 2025.
Huu ulikuwa mchezo wa 26 kwa Stars chini ya kocha huyu mzawa, tangu achukue timu hii Januari 2024 kwenye AFCON 2024 nchini Ivory Coast.
MP W D L GF GA GD PTS
26 12 7 7 23 17 5 43
Kwa matokeo haya, kocha Morocco anastahili kupongezwa kwani hakuna kocha yoyote wa Tanzania aliyewahi kupata matokeo kama haya kwenye mechi zake 26 kama hizi.
Tena hizi ni mechi ngumu na za ushindani kweli kweli ikiwemo kufuzu AFCON, fainali za CHAN na kufuzu Kombe la Dunia.
Morocco aliipokea timu kutoka kwa Adel Amrouche, Mfaransa mwenye asili ya Algeria, wakati wa AFCON 2024 ikiwa imeshacheza mechi moja
Morocco 3-0 Tanzania
Chini Hemed Suleiman Morocco. Stars ikapata sare mbili.
Zambia 1-1 Tanzania
Tanzania 0-0 DRC
Tena dhidi ya Zambia Stars ilikaribia kushinda kama sio Chipolopolo kusawazisha dakika ya mwisho.
Kwa sasa Taifa Stars ipo kwenye harakati za kufuzu Kombe la Dunia ikishinda nafasi ya pili nyuma ya vinara Morocco ambao wameshafuzu.
Tanzania inayo nafasi kubwa ya kumaliza wa pili kwenye kundi lenye timu ngumu ya Zambia yenye wachezaji wengi Ulaya na kocha mzoefu Avram Grant.
Matokeo ya leo kati ya Zambia na Morocco na ya kesho kati ya Tanzania na Niger, yatatoa picha nzuri zaidi kwa muelekeo wa kundi hili.
Lakini hata hivyo, Tanzania hadi sasa ila alama 10 ambazo ni za juu zaidi kujawahi kufikiwa katika harakati zote za nchi yetu kufuzu kwa mashindano yoyote.
Alama kama hizi Stars ilizipata kwenye harakati za kufuzu AFCON 2025, ilipomaliza ya pili nyuma ya DRC.
Na ni katika kipindi hiki ambacho kocha ni mzawa, Hemed Suleiman Morocco.
Lakini licha ya haya yote, Morocco anapokea ukosoaji mwingi wa kazi yake kuliko pongezi.
Wachambuzi wa mpira hawaangalii anachokifanya bali wanamhukumu kwa kile ambacho hakijafanyika.
Kikosi cha Stars kikitajwa, mjadala unakuwa kwa wachezaji ambao hawakuitwa kuliko walioitwa.
Badala ya kujenga morali ya kitaifa kuelekea mchezo husika, tunavunjana moyo kama taifa na kujitia unyonge.
Hapa ndipo kwenye msingi wa andiko hili. Haina maana kwamba Morocco anapatia kila kitu, hapana.
Yeye ni binadamu na utimilifu wa ubinadamu ni makosa lakini mwisho wa siku apimwe kwa kile anacholeta mezani, sio vinginevyo.
Imekuwa kawaida kwa wachambuzi kusema 'makocha wazawa hawana uwezo' bila kuangalia hao wazawa wanachokifanya kwa kulinganisha na makocha wageni ambao tumekuwa nao kwa miaka mingi.
Tanzania imeshakuwa na makocha wa kila aina lakini hakuna aliyefanya kama anachokifanya Hemed Morocco.
Kwa hiyo inapaswa tumuunge mkono kwenye hili anachokifanya katika wakati wake, kwa maslahi ya taifa letu.
Zambia wakiwa na Grant, kocha mkubwa aliyekaribia kutwaa ligi ya mabingwa Ulaya akiwa na Chelsea kama sio John Terry kuteleza kwenye penalti yake, anateseka kwa Morocco.
Yuko nyuma kwenye kundi kikiwemo kipigo cha 1-0 nyumbani kwao akiwa na wachezaji wake rundo kutoka Ulaya.
Guinea wakiwa na kocha wao Charles Paquille mwenye uraia wa Ufaransa pamoja na kundi la wachezaji wao kutoka vilabu vikubwa vya Ulaya, wamepigwa nje ndani na Stars chini ya mzawa Morocco.
Endapo Stars itamaliza ya pili kwenye kundi, itafuzu kwa mechi za mchujo (play off) ya Afrika kuelekea mchujo mwingine wa mabara kabla ya kufuzu kwa Kombe la Dunia.
Yaani baada ya mechi 6 za kufuzu Kombe la Dunia, Tanzania bado ina nafasi hii haijawahi kutokea hapo kabla.
Baada ya mechi kama hizi, Tanzania humaliza chini kwenye kundi na vialama vyake vichache.
Wakati.mwingine hutolewa hata kabla ya hatua ya makundi, katika miaka yenye mfumo huo.
Alama nyingi zaidi kuwahi kupata zilikuwa 8, kufuzu Kombe la Dunia 2010 ilipomaliza ya tatu nyuma ya Cameroon na Cape Verde.
Mashindano ya kufuzu Kombe la Dunia 2010, yalitumika pia kufuzu AFCON ya mwaka huo.
Ni kweli kwamba safari hii mfumo wa mashindano umebadilika na hatua ya makundi imekuwa na timu nyingi lakini hata hivyo, timu nyingi sio hoja, bali kushinda mechi.
Stars isingeshinda nyumbani kwa Zambia, ingekuwa nyuma tu hata kama timu ni nyingi.
Morocco anastahili kupongezwa kwa kazi nzuri anayoifanya.
ALIITWAJE MOROCCO
Watu wengi wanasikia tu kocha wa Taifa Stars anaitwa Morocco, lakini hawajui jina hili limetokea wapi.
Hemed Suleiman aliitwa Morocco kufananishwa na nyota wa Coastal Union, Hemed Salim Nassor almaarufu Morocco.
Alizaliwa Tanga mwaka 1957 na aliichezea Coastal Union miaka ya 1980 akiwa na akina Dancun Mwamba, Said George, Yassin Napili, Hussein Mwakuluzo na kadhalika.
Alianzia African Sports 1974 hadi 1976 na kuhamia Coastal Union kuanzia 1977 hadi 1988 alipostaafu.
Wakati Hemed huyu kocha wa Taifa Stars akianza kucheza soka, watoto wenzake wakamuita Morocco wakimfananisha na Hemed wa Coastal Union ambaye jina lake maarufu lilikuwa Morocco.
Jina hilo akakua nalo hadi akiwa Small Simba na Miembeni..na hadi sasa akiwa kocha mkubwa anayeweka historia.
Na yule Morocco wa Coastal Union aliitwa Morocco wakati akisoma shule ya msingi Mkwakwani.
Wanafunzi waligawanywa katika vikundi mbali vilivyopewa majina ya nchi mbalimbali za Afrika
Kila kikundi kiliunda timu ya mpira. Yeye akiangukia kikundi cha Morocco na akawa nahodha wa timu yake.
Kwa hiyo akawa anaitwa Hemed wa Morocco kwa maana ya Hemed nahodha wa kikundi cha Morocco.
Jina likakua na kumkaa, akazoeleka kama Hemed Morocco.
Hata alipoanza kucheza mpira ukubwani, jina likamng'ang'ania na akaendelea nalo, hadi likavuka bahari na kufika Zanzibar kwa Hemed Suleiman.