MO awarudisha watu wa mpira Bodi Simba

Mfanyabiashara Mohammed Dewji maarufu kwa jina la MO Dewji
Mwekezaji wa Simba Mohamed Dewji 'MO', amefanya uteuzi wa wajumbe wa bodi wa upande wake, akiwarudisha watu wa mpira ndani ya klabu hiyo.
Akitangaza uamuzi huo usiku huu, MO amesema kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa kwenye makubaliano na Simba ibara ya 40, amewateua Salim Mhene 'Try again',Mohamed Nassoro, Crescentius Magori,Hussein Kita, Zulfikar Chandoo na Rashid Shangazi.
Wajumbe hao wataingia kwenye bodi ya Simba wakiwa upande wa mwekezaji, ambapo ndani ya majina hayo sura tatu za Magori, Nassoro na Try again ni zile zilizokuwa kwenye bodi ya kwanza ya klabu hiyo zilizofanikisha Simba kuchukua mataji mara nne mfululizo.
Aidha, MO amesema baada ya mazungumzo ya muda mrefu, amekubali kujiuzulu kwa waliokuwa wajumbe Hamza Johari na Dk Raphael Chegeni.
"Baada ya kushauriana na Johari kwa muda mrefu, ameniomba apumzike kutokana na kubanwa na majukumu yake ya kikazi, hata hivyo nimemuomba abaki kwenye baraza la ushauri na amekubali," amesema MO.
"Pia Mwanasimba kindakindaki Raphael Chegeni ameniomba kupumzika kwa kuwa amekuwa yupo kwenye bodi nyingi mbalimbali naye amekubali kuingia kwenye baraza la ushauri."