Mmorocco azima tetesi za Fadlu Davids Afrika Kusini

Muktasari:
- Fadlu Davids ameiongoza Simba kufika hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2024/2025.
Orlando Pirates ya Afrika imezika rasmi tetesi za kumuwania kocha wa Simba, Fadlu Davids kuwa Kocha mkuu wa klabu hiyo baada ya leo Jumatatu, Juni 23, 2025 kumtangaza Abdeslam Ouaddou kuchukua nafasi hiyo.

Ouaddou ametangazwa kama mrithi wa nafasi iliyoachwa wazi na Jose Riveiro ambaye kwa sasa anaitumikia Al Ahly ya Misri.

Davids iliripotiwa kwamba alikuwa miongoni mwa makocha waliokuwa wakipewa kipaumbele cha kuchukua nafasi ya Riveiro baada ya Pirates kukoshwa na kazi aliyoifanya ndani ya Simba msimu huu.
Davids ameiongoza Simba kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika katika msimu wa 2024/2025 ambapo ilipoteza kwa mabao 3-1.

Riveiro alijiunga na Ahly baada ya kuiongoza Orlando Pirates kufika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambayo walipoteza dhidi ya Pyramids FC.
Ouaddou ambaye ana umri wa miaka 47, ni kocha mwenye uzoefu mkubwa wa soka alioupata kwa kucheza na pia katika taaluma ya ukocha.

Kocha huyo ameichezea timu ya taifa ya Morocco idadi ya mechi 68 na anasifika kwa uwezo wake mkubwa wa uongozi mzuri wa wachezaji.
Taarifa ya Orlando Pirates imefafanua kwamba Ouaddou atasaidiwa na Mandla Ncikazi, Rayaan Jacobs, Helmi Gueldich na Tyron Damons.
“Uwezo wake mkubwa wa kuuelewa mchezo na wasifu wake wa kiuongozi unamuweka katika nafasi nzuri ya kuiongoza Buccaneers katika zama mpya,” imesema taarifa ya Pirates.

Kabla ya kujiunga na Pirates, Ouaddou amewahi kuzifundisha Marumo Gallants, AS Vita Club, timu ya Taifa ya Algeria Loto na MC Oujda.
Klabu ambazo Ouaddou amewahi kuzichezea kabla hajastaafu soka ni Nancy, Fulham, Rennes, Olympiacos, Valenciennes, Al Duhail na Qatar SC.