Prime
Mkataba mpya Job kizungumkuti, meneja afunguka

Muktasari:
- Dickson Job alijiunga na Yanga katika dirisha dogo la usajili, Januari 2021 na msimu wa 2022/2023 aliibuka mshindi wa tuzo ya beki bora wa Ligi Kuu.
Beki tegemeo na nahodha msaidizi wa Yanga, Dickson Job ni miongoni mwa baadhi ya nyota wa timu hiyo ambao mikataba yao ya kuitumikia itafikia ukingoni mwishoni mwa msimu huu.
Nyota huyo alisaini mkataba wa miaka miwili mwaka 2023 na msimu huu utakapomalizika atakuwa huru kujiunga na timu nyingine yoyote kama kanuni ya usajili ya Bosman inavyoruhusu.
Wakati siku zilizobaki za mkataba wa Job na Yanga zikibakia chache, meneja wa beki huyo, George Job amefunguka juu ya hatima ya mchezaji wake klabuni hapo huku akifichua kuwa mambo hayajakaa sawa hadi sasa.
George Job amesema kuwa hakuna kinachoendelea katika suala la mkataba mpya baina ya Yanga na Dickson Job hivi sasa na upande wa mchezaji umeuacha mpira kwa uongozi wa klabu hiyo.
"Dickson Job bado hajasaini mkataba mpya wa kuendelea kuichezea Yanga na mazungumzo baina yetu na klabu hayajafika mwisho kwani kwa muda mrefu sasa yamesimama," amesema George Job.
Meneja huyo wa Job amesema kuwa zipo ofa za timu nyingine zikimhitaji mchezaji huyo hivyo kama wasipofikia muafaka na Yanga watazipa kipaumbele.
"Kuna ofa kwa timu za ndani na nje ya nchi lakini kiutaratibu, klabu ambayo mchezaji anaichezea ndio inapewa kipaumbele cha kwanza na mkishindwa kufikia makubaliano ndio mnazifanyia kazi ofa nyingine," amesema meneja huyo.
Ofisa habari wa Yanga, Ally Kamwe ameiambia Mwananchi Digital kuwa ni kweli mkataba wa Job na baadhi ya wachezaji inaelekea ukingoni na klabu inafanya mazungumzo kwa ajili ya mikataba mipya.
"Tuko kwenye mazungumzo na hao wachezaji na sio kweli kwamba wamesaini mikataba mipya," amesema Kamwe.
Job alijiunga na Yanga, Januari 2021 na tangu hapo mchezaji huyo amekuwa tegemeo la safu ya ulinzi ya timu akiwa nahodha msaidizi ambapo amekuwa akicheza mara kwa mara sambamba na beki mwingine wa kati, Ibrahim Hamad 'Bacca'
Kiwango bora ambacho Job amekionyesha akiwa na kikosi cha Yanga, kimemfanya pia awe miongoni mwa wachezaji chaguo la kwanza katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars'
Kwa misimu mitatu mfululizo iliyopita, Job amefanikiwa kuingia katika kikosi bora cha msimu cha Ligi Kuu na katika msimu wa 2022/2023 alifanikiwa kuibuka mshindi wa tuzo ya beki bora wa Ligi Kuu.
Job alijiunga na Yanga akitokea Mtibwa Sugar ambayo nayo ilimnasa kutoka katika kituo cha kuibua, kulea na kukuza vipaji vya soka kwa vijana wadogo cha Moro Kids kilichopo mkoani Morogoro.
Beki huyo kwa sasa ana umri wa miaka 24, amechezea timu za taifa za umri wa ngazi zote kuanzia ile ya umri wa miaka 17 'Serengeti Boys' hadi ya wakubwa.