Mechi ya hesabu Taifa Stars
Muktasari:
- Katika mechi sita zilizopita hivi karibuni, Taifa Stars imepata ushindi mara tatu, imetoka sare mbili na kupoteza moja tu.
Dar es Salaam. Dakika 90 za mchezo wa leo dhidi ya Niger kwenye Uwanja wa New Amaan Complex Zanzibar zina maana kubwa kwa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' katika harakati zake za kusaka tiketi ya kucheza mechi za mchujo za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026.
Baada ya kukosa tiketi ya moja kwa moja ya kushiriki Kombe la Dunia mwakani kwa kushindwa kuongoza kundi lake E ambalo kinara ni Morocco, nafasi pekee ambayo Taifa Stars inaweza kuipata ni kupitia hatua ya mchujo kwa kuanzia kanda ya Afrika na kisha baadaye kidunia.
Na hili hilo la mchujo lifanikiwe, kuna ulazima wa kuibuka na ushindi leo ili ifikishe pointi 13 hivyo itabakia na mchezo mmoja dhidi ya Zambia ambayo ikipata ushindi itajihakikishia kumaliza katika nafasi ya pili ya kundi E ikiwa na pointi 16.
Kwa Afrika, baada ya hatua ya makundi kuwania kufuzu Kombe la Dunia kumalizika, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika limeweka utaratibu wa kupunguza pointi ambazo timu zote zilizo katika makundi yenye timu sita ambazo zilipata dhidi ya timu zilizoshika mkia kwenye makundi hayo ili kupata uwiano na timu zilizoshika nafasi ya pili katika makundi yenye timu chache.
Tanzania ikiwa itamaliza katika nafasi ya pili na kama itashinda mechi zake mbili zilizobakia dhidi ya Niger na Zambia ambazo zote itacheza nyumbani, itakuwa ni miongoni mwa wanufaika kwa vile yenyewe haitopunguziwa pointi zake kwa sababu kundi lake lina timu chache kulinganisha na mengi ambapo lina timu tano.
Kwa sasa timu nne zilizo juu katika chati ya timu zenye idadi kubwa ya pointi zinazoshika nafasi ya pili Gabon ndio kinara ikiwa na pointi 17 ikifuatiwa na Cameroon yenye pointi 15 sawa na Senegal iliyo nafasi ya tatu na Burkina Faso inafuatia ikiwa na pointi 14.
Hata hivyo, Burkina Faso, Cameroon, Senegal na Gabon zote zipo katika makundi yenye timu sitasita kila moja kulinganisha na Taifa Stars ambayo ipo kwenye kundi lenye timu tano.
Kocha mkuu wa Taifa Stars, Hemed Morocco amesema kuwa bado wana matumaini makubwa ya kupata nafasi ya kucheza mechi za mchujo.
“Hatujapata matokeo ambayo tuliyategemea dhidi ya Congo lakini pointi moja tuliyopata ni muhimu. Nafasi tunayo ya kucheza hatua ya mchujo kama tutashinda mechi mbili zilizobakia.
“Tutajitahidi kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika mechi ya Congo ili tufanye vizuri katika mchezo unaokuja dhidi ya Niger,” alisema Morocco.
Kumbukumbu zinaonyesha Taifa Stars imekuwa na historia nzuri katika michezo yake dhidi ya Niger ambapo katika mechi tatu walizokutana, imepata ushindi mara mbili na kutoka sare moja.
Lakini pia Taifa Stars inaingia katika mechi ya leo ikiwa na mwenendo mzuri kulinganisha na wapinzani wao Niger.
Katika mechi sita zilizopita hivi karibuni, Taifa Stars imepata ushindi mara tatu, imetoka sare mbili na kupoteza moja tu.
Niger yenyewe katika mechi sita zilizopita, haijapata ushindi na imetoka sare tatu huku ikipoteza mechi tatu.