Mbappe, Vinicius na Rudger hatihati kuikosa Arsenal

Muktasari:
- Nyota wa Madrid wamekuwa na mikasa mibaya msimu huu kwani siku chache zilizopita Jude Bellingham alifungiwa kutocheza michezo miwili ya La Liga kwa kosa la utovu wa nidhamu.
Madrid. Nyota wa Real Madrid Antonio Rudiger, Kylian Mbappe, Dani Ceballos na Vinicius Junior wanachunguzwa na UEFA kwa tuhuma mbaya za ushangiliaji baada ya ushindi wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Atletico Madrid.
Picha za televisheni zilimuonyesha Rudiger akifanya ishara ya kukata shingo kuelekea kwa mashabiki wa Atletico Madrid, huku Mbappe akionekana kushika sehemu zake za siri.

Katika mchezo huo Vinicius alionekana kuonyesha ishara ya namba 15 na sifuri akiwaonyesha mashabiki wa Atletico Madrid ambapo 15 ni jumla ya mataji ya UEFA iliyonayo Madrid wakati sifuri ni Atletico Madrid ambayo haijawahi kutwaa taji hilo.
Kitendo hicho kilichukuliwa kama ishara ya uchochezi kwa mashabiki wa Atletico Madrid.
Kwa mujibu wa jarida la Sky Sports la Machi 27, 2025 linaeleza kuwa nyota hao wa Real Madrid wapo katika uchunguzi ambapo Shirikisho la soka Barani Ulaya (UEFA) tayari limeanza kufanya uchunguzi kwa kurejea video zinazowaonyesha wachezaji hao wakishangilia mwishoni mwa mchezo.
Katika mchezo huo Madrid ilipata ushindi baada ya changamoto za mikwaju ya penati 4-2 na kufanikiwa kufuzu kwenye hatua ya robo fainali.

Hata hivyo inaaminika kwamba huwenda nyota hao wakapewa faini tofauti na kile watu wanachoamini kuwa rabda wakafungiwa kucheza michuano hiyo ambapo Madrid watakutana na Arsenal katika hatua ya robo fainali.
Mwaka 2019 UEFA ilimpiga faini Christiano Ronaldo alipokuwa na Klabu ya Juventus baada ya kufanya kitendo kisichofaa wakati aliposhangilia bao kwenye mchezo dhidi ya Atletico.
Ronaldo alitozwa faini ya Euro 20000 (Sh57 bilioni) ikiwa sawa na faini aliyotozwa kocha wa Atletico Madrid, Diego Simeone ambaye naye alishangilia kimakosa katika mchezo wa kwanza uliochezwa Hispania ambapo Atletico ilipata ushindi wa mabao 2-0.
Madrid itarejea kwenye uwanja wa Emirates Aprili 8, 2025 katika mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la UEFA ambapo mara ya mwisho timu hizo zilikutana Machi 8, 2006 ambapo mchezo ulimaliza kwa sare ya bila kufungana.
Katika msimu huo Arsenal ilisonga mbele kwani ilikuwa imetoka kushinda ugenini ambapo iliifunga Madrid bao 1-0 kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu.