Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Madaktari wa kike hatarini kujiua

Muktasari:

  • Tanzania ina jumla ya madaktari 14,000 waliosajiliwa na Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) wakiwemo 600 wa upasuaji, huku zaidi ya 5000 wakitajwa kuwa vijiweni (hawana ajira).

Dar es Salaam. Leo Machi 30 dunia ikiadhimisha siku ya madaktari duniani, Ripoti mpya inaonyesha madaktari wa kike wana uwezekano wa asilimia 76 zaidi ya kufariki dunia kwa kujiua ikilinganishwa na wanawake wengine.

Madaktari hutumia zaidi ya miaka saba kupata maarifa chuoni na hutumia sehemu kubwa au yote ya maisha yao kutoa huduma za afya usiku na mchana.

Taarifa iliyotolewa leo Jumapili, Machi 30, 2025 na Shirika la Afya Duniani (WHO), imeeleza mzigo mkubwa wa kazi, mishahara midogo, mazingira hatarishi na unyanyapaa huwafanya wengi kuteseka kimyakimya.

Imeeleza WHO inaheshimu kujitolea kwa madaktari kote duniani, huku ikitambua janga tulivu linalowakumba.

Amesema madaktari duniani wanakabiliwa na viwango vya juu vya kuchoka kazini, msongo wa mawazo, wasiwasi na hata kujiua. Wanajitolea maisha yao kuponya wengine, lakini afya yao ya akili mara nyingi haizingatiwi.

"Ripoti inaonyesha madaktari wa kike wana uwezekano wa asilimia 76 zaidi wa kufariki kwa kujiua ikilinganishwa na wanawake wengine.

"Mpaka sasa ni asilimia 35 pekee ya nchi zinazoendesha mipango ya kitaifa ya kusaidia afya ya akili inayohusiana na kazi. Tuitumie siku hii kuongeza uelewa na kusherehekea madaktari kote duniani kwa huduma na kujitolea kwao kila siku," imeeleza taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Kutokana na ongezeko la watu duniani na kada hiyo kutopewa umuhimu, WHO inaonya juu ya upungufu wa wahudumu wa afya milioni 11 ifikapo mwaka 2030.

Uhalisia nchini

Licha ya changamoto kadhaa zinazoikabili kada hiyo nchini, bado kutotosheleza kwao, huwalazimu kufanya kazi kupita kiasi na hivyo kutumia muda mwingi kazini.

Madaktari wa upasuaji huathirika zaidi hasa kada nyeti, kwa mujibu wa Rais wa chama cha madaktari wa upasuaji Tanzania, Dk Amani Malima kuna idadi ya wataalamu hao 600 pekee nchini.

Kwa mujibu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), nchini kuna madaktari waliosajiliwa 14,000 na Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT).

"Nchini Tanzania Madaktari wanafanya kazi usiku na mchana kuokoa maisha ya watu katika vituo vya kutolea huduma, wanatimiza wajibu huu mkubwa na adhimu kwa kujitoa mno," amesema Rais wa MAT, Dk Mugisha Nkoronko katika taarifa yake.

Amesema madaktari wanatumia muda mrefu kupata maarifa wakati wakisoma, na wanatumia sehemu kubwa au yote ya maisha yao kutoa huduma stahiki za afya kwa wote wanaozihitaji.

Amesema madaktari wametoa maisha yao kuwa sadaka kwa wananchi wanaopokea huduma zao. Na kwamba wito wao haupimiki.

"Madaktari ni askari wa mstari wa mbele katika vita ya kupambana na adui maradhi, ni viongozi katika maendeleo muhimu ya sekta ya afya na ustawi wa Taifa letu.

"Ninawatakia afya njema na maisha marefu madaktari wote nchini. Ninawakumbusha kutimiza majukumu yao kwa weledi na maadili ya hali ya juu," amesema Dk Nkoronko.

Pamoja na hayo amewahakikishia MAT itaendelea kulinda taaluma ya udaktari kwa wivu mkubwa.

Amesema licha ya changamoto zilizopo kada hiyo itaendelea kutimiza wajibu wake kikamilifu, kila wakati usiku na mchana wakati wote.

Wito

Dk Nkoronko ameziomba mamlaka zote zinazohusika ikiwemo Serikali, kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa madaktari kutimiza wajibu wao na kuwafanya wananchi kote nchini kupata huduma bora za afya.

"Waendelee kuboresha maslahi yao, ikiwemo vitendea kazi na mambo mengine yanayoboresha ustawi wao, kama watu muhimu katika jamii.

"Ninawakumbusha kuendelea kujali afya zao pia maana kazi hii inatuweka kazini masaa mengi, tunakosa muda wa kujihudumia binafsi na kupata msongo, na matatizo ya afya ya akili.

"Nasi pia tunaugua wakati mwingine tunaambukizwa magonjwa na tunaowahudumia. Ni muhimu nasi tuendelee kujikinga kwa magonjwa yote ya tabia bwete na ya kuambukizwa," amesema Dk Nkoronko.