Mastaa Simba: Tuleteeni Fei Toto

Magwiji wa Simba wamesema kama Feisal Salum 'Fei Toto' atamaliza kesi yake na Yanga ni mtu sahihi pale Msimbazi msimu ujao; "ana nafasi ya kumtoa mtu Simba akacheza."

Fei Toto yupo kwenye mvutano na mabosi wake juu ya mkataba, ambapo anataka uvunjwe ili aangalie maisha ndani ya klabu nyingine kutokana na kile anachodai kuwa ni maslahi duni na pia hana furaha ndani ya Yanga. Klabu hiyo imemshtaki kwenye mamlaka za Soka na kuna shauri linaendelea.

Emmanuel Gabriel 'Batgol', Henry Joseph na Joseph Kaniki 'Golota' ambao wameng'ara na Simba kwa nyakati tofauti, wamekiri kwamba pamoja na mambo mengine bado umri wake unamruhusu kung'ara lakini Simba wasubiri suala la Fei na mabosi wake linamalizika punde.

Batgol ambaye alijijengea heshima kwa kuinyanyasa Yanga kwenye mechi za watani, alisema; "Simba wakimsajili Fei watakuwa na bahati na wamelamba dume, pia atawachangamsha Simba na ataleta ushindani ndani ya timu,ana nafasi ya kumtoa mtu akacheza.

"Kikubwa amalizane na Yanga vizuri ili anakoenda awe huru, namwamini kuwa ni miongoni mwa wachezaji ambaye anaweza kufanya mabadiliko makubwa kwenye timu."

Naye Kaniki alisema; "Kwanza Fei umri wake ni mdogo na ana kipaji, hakuna asiyefahamu hilo, kama watabahatika kumsajili basi litakuwa jambo jema na Fei ana uwezo wa kucheza kwa kocha na timu yoyote ni suala la mfumo tu.

"Fei yupo kwenye kiwango kizuri na kinapanda, hizi zingine ni changamoto ambazo wengi wamewahi kuzipitia na maisha yako hivyo, kikubwa anapaswa kuwa na washauri wazuri na wenye kuujua mpira na mikataba ya mchezaji kisoka ikoje na  watakaomsaidia kulimaliza jambo lake wengine waendelee kuwa walezi wake.

"Hadi sasa Fei kwa mujibu wa mkataba wake bado ni mchezaji wa Yanga na anapaswa kuuheshimu na hata kama mkataba wake ungekuwa unamalizika msimu huu angekuwa ndani ya kiwango bora kisoka, uwezo wake ni mkubwa," alisema Kaniki ambaye ni mchezaji wa zamani wa Mtibwa.

"Ikumbukwe tu kwamba Simba na Yanga sio mwisho wa maisha ya soka, mpira wa sasa ni sayansi, wachezaji wanapaswa kuingia mfuko na kutoa pesa kwa ajili ya kuwa na watu makini wa kuwasimamia kwenye mambo yao kisoka, suala la Fei tunaombea liishe salama kwani anahitajika sana hata kwenye Taifa."

Henry ambaye aliwahi kucheza Canada, alisema kuwa Fei ni mchezaji mzuri na ana uwezo wa kucheza Simba kikosi cha kwanza lakini mabosi wao wa Wekundu hao wasitumie nguvu sana kwenye usajili wa Fei bali kipindi kama hiki waangalie hata sehemu nyingine kwani kuna wachezaji wazuri.

"Fei anaweza kucheza na kuisaidia Simba lakini kwasasa haina sababu kutumia nguvu kubwa kupata saini yake, kikubwa ni kumuombea ili tatizo lake na mabosi wake limalizike ndipo wao wamsajili akiwa hana shida na klabu yake.

"Nafasi ya Fei ipo wazi pale Simba itategemea tu na mfumo ambao kocha atautumia, anaweza kumchezesha Clatous Chama pembeni halafu Fei akacheza kama namba 10, hata akiwatumia pamoja na Saido Ntibanzokiza anacheza tu.

"Simba wanaweza kuwekeza nguvu sehemu nyingine, maana wachezaji wapo wengi wazuri ila ni kuwaamini tu, kama wanahitaji huduma ya Fei wakati kesi yake haijamalizika wanawaze kuchelewa muda wa usajili ukapita. Kikubwa tunamuombea Fei na tunatamani kuona amerudi uwanjani, si klabu tu kumtegemea kwani hata Taifa linamtegemea," alisema Henry.