Mashabiki Simba wabebeshwa faini ya CAF

Muktasari:
- Simba inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi A la Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa na pointi 10.
Dar es Salaam. Siku moja baada ya kutangazwa kwa adhabu ya kuizuia Simba kucheza bila mashabiki katika mechi yake ya mwisho ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Constantine katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili, sambamba na faini ya Dola 40,000, Simba imeweka utaratibu maalum kwa mashabiki wao kuisaidia kulipa faini hiyo.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema kuwa kuanzishwa kwa utaratibu huo kumetokana na maombi ya mashabiki wenyewe wa Simba.
"Kuelekea mchezo wa Jumapili, Simba Sports Club tumepata pigo la kubwa na pigo lenyewe ni kuzuiliwa kuingiza mashabiki katika mchezo wetu. Tunasema pigo kwa kuwa tunafahamu nguvu kubwa ya mashabiki wanapokuwepo uwanjani. Hao mashabiki bora ambao tunajinasibu nao hawatakuwepo uwanjani Jumapili hii.
"Taarifa sahihi ni tumefungiwa mechi moja, mechi ya robo fainali tutacheza na mashabiki na tayari sisi tumeshafuzu. Baada ya hukumu kutoka yameibuka maoni mengi ya mashabiki wakitaka ushirikishwaji kwa kuwa kosa hili ambalo limetokea ni la Wanasimba wote, asitokee wa kumnyoshea kidole mwenzake.
"Tumekuja na kampeni maalumu ambayo hii imeombwa na amshabiki wenyewe wakitaka kuwajibika baada ya kufanya makosa yale. Tumewaletea mfumo wa kuchangia ili kitakachopatikana twende tukalipe faini na Simba Sports Club ibaki salama. Kampeni hiyo tumeipa jina la TUNAWAJIBIKA PAMOJA,” amesema Ahmed Ally.
Ahmed alisema kuwa mchango huo utumwe moja kwa moja katika namba ya klabu.
“Natoa rai kwa Wanasimba, asijekutokea Mwanasimba wa kuchangisha kwamba kikifika kiasi fulani tutapeleka ofisini. Kila Mwanasimba atume fedha yake moja kwa moja kwenye namba ya ofisi ambayo imetolewa.
"Zoezi letu tumeliweka kwa muda sio kwa kiwango kwahiyo kama ikifika milioni 100 na muda bado tutawaachia. Wanasimba wanapaswa kuonyesha nguvu yao, wanapaswa kusimama na timu yao,” amesema Ahmed Ally.