Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kinachoisubiri Simba, Sfaxien vurugu kwa Mkapa

Muktasari:

  • Simba inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi A la Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa na pointi sita sawa na vinara Onze Bravos na CS Constantine inayoshika nafasi ya pili na CS Sfaxien inashika mkia ikiwa haina pointi.

Dar es Salaam. Vurugu zilizotokea katika mechi ya Kombe la Shirikisho baina ya Simba na CS Sfaxien ya Tunisia jana katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam zinaweza kusababisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) kutoa adhabu kubwa mbili kwa timu hizo.

Adhabu hizo mbili ni faini ya fedha na nyingine ni kifungo ambacho kinaweza kuwa cha mechi au kutojihusisha na shughuli za mpira wa miguu.

Mchezo huo ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1, haukumalizika salama kutokana na fujo zilizotokea ambazo zilipelekea kung'olewa kwa viti 256 vya uwanja huo, kuumia kwa shabiki mmoja na kupigwa kwa refa wa mechi hiyo, Andofetra Rakotojaona kutoka Madagascar.

Adhabu ambayo Simba haina namna ya kukwepa ni kulipa fidia ya uharibifu uliofanyika uwanjani hapo kwa vile yenyewe ndio ilikuwa mwenyeji na ndio ambayo imeukodi kwa ajili ya matumizi yake ya kucheza mashindano ya kimataifa.

Tayari wizara ya habari, utamaduni, sanaa na michezo umeshatoa taarifa ya kuitaka Simba ihakikishe inalipa gharama za uharibifu ambao umetokea juzi uwanjani hapo.

"Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuchukua hatua mara moja kwa kuwaandikia timu ya Simba Sports Club na kuwanakili Shirikisho la Kandanda Tanzania (TFF) ili gharama za uharibifu uliosababishwa katika mechi hiyo zilipwe," ilifafanua taarifa hiyo ya wizara.

Ukiondoa kuilipa serikali gharama ya uharibifu wa viti, Simba inaweza kujikuta ikikumbana na adhabu ya faini isiyozidi Dola 10,000 ikiwa itabainika mashabiki wake kuhusika na vurugu hizo kwa vile litakuwa tukio la kwanza la kung'oa na kurusha viti uwanjani kufanywa na mashabiki wake kwenye mechi za mashindano ya klabu Afrika.

Rungu kubwa linaweza kuiangukia CS Sfaxien kutokana na idadi kubwa ya makosa ambayo iliyafanya kama timu katika mchezo wa juzi pamoja na mashabiki wake na ambayo yalichangia kwa kiasi kikubwa vurugu zilizotokea juzi.

Kosa la kwanza ni bughudha ambayo wachezaji na maofisa wake wa benchi la ufundi lilifanya kwa marefa na maofisa wengine wa mchezo huo wakati na baada ya mchezo na mfano ni tukio la kuvamiwa na kupigwa kwa refa Rakotojaona baada ya mchezo kumalizika.

Mbali na hilo, picha mbalimbali za video zilionyesha mashabiki wa CS Sfaxien wakipigana na maofisa wa timu hiyo katika vyumba vya kubadilishia nguo mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo.

Maofisa hao wa benchi la ufundi na wachezaji wa Sfaxien mbali na vurugu kwa refa pia waliwapiga na kuwarushia makopo ya maji maofisa usalama uwanjani pindi walipojaribu kuwazuia kufanya vurugu katika mechi ya juzi.

Mashabiki hao pia walihusika katika kung'oa viti na kuvirusha uwanjani pamija na kupigana na mashabiki wa Simba na walinzi wa uwanjani jambo lililopelekea mmojawapo kuumia.

Kosa lingine ambalo lilifanywa na mashabiki hao wa Sfaxien ni kuonyesha ishara za kisiasa baada ya kupeperusha bendera za Palestina jambo ambalo ni kinyume na katiba na miongozo ya Shirikisho la mpira wa Miguu Afrika (Caf).

Picha mbalimbali za matukio ya vurugu baada ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, uliowahusisha wenyeji Simba SC dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia.

Kwa mujibu wa ibara ya 49 ya katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf), hairuhusiwi uonyeshwaji wa jumbe zenye mlengo wa kisiasa katika eneo kunakofanyika tukio la kimashindano.

“Hakuna uonyeshwaji wowote wa kisiasa, kidini au propaganda za kibaguzi ambao unaruhusiwa katika eneo la kimashindano la Caf,” inafafanua ibara hiyo.

Muda wa mapumziko, walitembeza bendera kubwa ya nchi hiyo katika jukwaa la upande wa Kaskazini ambako walikuwa wamekaa.

Wakati wakifanya hivyo, ofisa habari wa Caf kwenye mechi hiyo, Ahmed Hussein kutoka Uganda ameonekana akipiga picha kwa simu yake ya mkononi tukio la mashabiki hao kupeperusha bendera hizo, ikionekana kama kuchukua ushahidi wa jambo hilo.

Kwa mujibu wa kanuni za nidhamu za Caf, mchezaji au ofisa wa timu anayefanya kosa la kumshambulia refa au ofisa wa mchezo anaweza kufungiwa kuanzia idadi ya mechi nne hadi miezi sita na kupewa adhabu ya kuanzia Dola 5000.

Kosa la vurugu linalofanywa na timu nzima linaweza kupelekea adhabu ya faini inayoweza kufikia hadi Dola 300,000 na isiyopungua Dola 50,000 kutegemeana na uzito na ukubwa wa kosa lenyewe.

Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Angetileh Osiah alisema kwa mazingira ya vurugu za juzi, timu zote mbili zitakutana na adhabu.

"Simba wao watatakiwa kulipa hasara iliyotokea kwa Mkapa kwa sababu wao ndio walikodi uwanja na wanatakiwa kuurudisha ukiwa kama walivyoukuta, Shirikisho haliwezi kuidai CS Sfaxien.

"Mengi yanazungumzwa kuhusiana na tukio la jana (juzi) kuhusu suala la Simba kufungiwa kuingiza mashabiki sioni hilo likitokea wala hawawezi kupokea adhabu yoyote kutoka Caf labda CS Sfaxien na wao sio kufungiwa watapigwa faini," alisema Osiah.

Picha mbalimbali za matukio ya vurugu baada ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, uliowahusisha wenyeji Simba SC dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia.

Ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally alisema klabu yake inaalani vurugu za juzi na

"Sisi Simba tunaalaani aina yoyote ya vitendo vya vurugu katika viwanja vya mpira wa miguu. Mamlaka zote za usimamizi wa mchezo wameona wamechukua ripoti naamini wataenda kuwasilisha katika mamlaka za juu zaidi ili tuweze kujua kitu gani kinafanyika.

Vitendo vya vurugu uwanjani ni vitendo visivyokubalika hasa katika soka la kisasa na tunaamini mamlaka zitatoa uamuzi wa haki," alisema Ahmed Ally.