Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mabeki, viungo silaha muhimu Simba

Dar es Salaam. Katika hatua nyingine ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba SC ina kibarua kizito leo Jumapili cha kukabiliana na CS Sfaxien kutoka Tunisia. Mchezo huu utapigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, na unatarajiwa kuwa na mvuto mkubwa kutokana na umuhimu wake kwa pande zote mbili.

Simba, ikiongozwa na kocha Fadlu Davids, inahitaji ushindi ili kuimarisha nafasi yao katika Kundi A na kuweka matumaini yao ya kusonga mbele hatua ya robo fainali.

Simba SC, ambayo kwa sasa inashika nafasi ya pili kwenye Kundi A, inajivunia ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Bravos do Maquis lakini pia wamekumbwa na kipigo cha 2-1 ugenini dhidi ya CS Constantine. Hivyo, ushindi dhidi ya CS Sfaxien ni muhimu sana kwao, kwani utawapa matumaini ya kujisogeza katika nafasi nzuri ya kufuzu robo fainali.

Simba ina wachezaji wenye uwezo mkubwa ambao Kocha Fadlu Davids anajivunia nao huku akiitaja safu ya ulinzi na kiungo imekuwa nguzo muhimu zaidi.

“Ni kawaida kwamba tunajitahidi kuendelea kuwa na safu imara ya ulinzi, sio Che Malone (Fondoh) na Hamza (Abdulrazack) pekee kama angekuwa na afya nzuri, bali Chamou (Karaboue), Hamza na Che Malone, hawa watatu ni sehemu ya safu hiyo kuu. Pia Fabrice (Ngoma) hivi karibuni amekuwa mchezaji muhimu katika kudhibiti timu katikati ya uwanja,” alisema Fadlu.

Akizungumzia mchezo huo, Fadlu alisema: "Tunahitaji pointi tatu, hii ni mechi muhimu na ngumu ambayo tunatakiwa kushinda, tumekuwa na wakati mzuri wa kujiandaa, kama nilivyosema mwanzo tutakuwa na mabadiliko ya kimbinu tofauti na mchezo uliopita."

Kwa upande mwingine, CS Sfaxien wanakuja wakiwa na presha kubwa baada ya kupoteza michezo miwili mfululizo, mmoja wakiwa nyumbani dhidi ya CS Constantine (1-0) na nyingine ugenini dhidi ya Bravos do Maquis (3-2).
Kuna mambo kadhaa yanayoweza kuipa Simba SC nafasi nzuri ya kuibuka na ushindi katika mchezo huu ambayo ni:


Mabeki wa kati

Ukuta wa Simba unategemea sana mabeki wake wa kati, ambao wamekuwa na uwezo mkubwa wa kutuliza mashambulizi ya wapinzani. Che Malone Fondoh, Abdulrazack Hamza na Chamou Karaboue ni mabeki wa kati wa Simba ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha timu inakuwa na ulinzi imara.

Katika mechi nyingi, mabeki hawa wameweza kuzuia mashambulizi ya hatari kutoka kwa timu pinzani na kuhakikisha kipa wao, Moussa Camara anapata utulivu golini.

Kwenye mchezo dhidi ya CS Sfaxien, mabeki wa Simba wanahitaji kuwa makini zaidi dhidi ya wachezaji hatari kama Hazem Haj Hassen mwenye mabao mawili katika michezo miwili iliyopita na Firas Sekkouhi. Hazem, ambaye ni mchezaji wa kimataifa kutoka Tunisia, ni tishio kubwa kwenye mashambulizi ya juu, hivyo mabeki wa Simba wanahitaji kuhakikisha wanachukua hatua za haraka ili kumzuia. Ikiwa mabeki wa Simba wataweza kuzuia mashambulizi ya CS Sfaxien, basi timu itakuwa na nafasi nzuri ya kushinda.


Nguvu ya kiungo

Simba SC ina viungo muhimu ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika mwenendo wa timu hiyo. Fabrice Ngoma ni moja ya silaha kubwa katika safu hiyo ya Simba licha ya awali kutatizika kuingia kwenye mfumo wa Fadlu.

Ngoma ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kupiga pasi fupifupi na ndefu kwa usahihi, kuanzisha mashambulizi na kuzuia mipira ya wapinzani.

Pia, Jean Charles Ahoua mwenye mabao matano na asisti nne katika ligi ni kiungo mwingine muhimu kwa Simba, hasa akiwa na mchango mkubwa katika kutengeneza mabao. Ahoua anajulikana kwa uwezo wake wa kupiga pasi za hatari na kuwaongoza wenzake wakiwa katika maeneo ya hatari. Uwezo wa Ahoua katika kuunda nafasi za mabao unaweza kuwa na umuhimu mkubwa katika mchezo huu.

Ikiwa Ngoma, Augustine Okejepha au Debora Mavambo na Ahoua wataendelea kufanya vizuri, basi Simba itakuwa na nguvu kubwa ya kutengeneza mashambulizi hatari dhidi ya CS Sfaxien.


Ushambujiaji

Wachezaji wa mbele wa Simba, Leonel Ateba na Steven Mukwala ni sehemu ya mpango wa mashambulizi ya Simba itategemea na Fadlu atahitaji kuanza na nani kati yao kwenye eneo la mwisho, bado washambuliaji hao ni kama wanajitafuta.

Hivyo mechi hii inamuhitaji Mukwala au Ateba akiwa kwenye kiwango kizuri, ni mechi ambayo inaweza kuwa na nafasi chache hivyo inahitaji kuwa na wastani mzuri wa kutumia nafasi ambazo zinaweza kutengenezwa.  

Kuwa katika boksi kwa wakati ni jambo muhimu ambalo litahitaji kwa mshambuliaji wa mwisho kutokana na nguvu ya mashambulizi ambayo Simba ipo nayo katika maeneo yake ya pembeni ambapo mabeki Shomary Kapombe na Mohammed Hussein 'Tshabalala' wamekuwa wakihusika kwa kupiga krosi au pasi mpenyezo.

Mbali na kutegemea mshambuliaji wa mwisho katika kuamua matokeo, Simba ina faida ya kuwa na wachezaji kutoka maeneo mengine wenye uwezo wa kufunga mfano mzuri ni Ahoua mwenye mabao matano na asisti nne katika ligi.


Mbinu Kimchezo

Fadlu ameonyesha kupendelea mfumo wa 4-2-3-1, ambao ni wa soka la kisasa unaotumika sana. Mfumo huu unawaruhusu viungo wa kati wa Simba kuwa na udhibiti mkubwa wa mchezo na kuwa na ufanisi mkubwa katika kushambulia na kulinda.

Katika mfumo huu, viungo wawili wa ulinzi, kama vile Ngoma na Okejepha, wanahakikisha kuwa Simba inaendelea kuwa imara kwenye eneo la kati, huku wakiwazuia wachezaji wa CS Sfaxien kufanya mashambulizi.

Kwa mbele, viungo wa kushambulia kama Kibu Denis, Ladaki Chasambi na Ahoua wanapata nafasi nzuri ya kushambulia na kutengeneza nafasi za mabao. Mfumo wa 4-2-3-1 pia unawawezesha wachezaji wa pembeni kuingia kwenye maeneo ya hatari kwa haraka na kuleta madhara kwenye lango la wapinzani.

Ikiwa Fadlu atatumia mfumo huu vizuri, utaweza kuwa na mafanikio makubwa kwa Simba, hasa ikizingatiwa kuwa wachezaji wa Simba wamezoea mfumo huu na wanaufahamu vyema.


Faida ya nyumbani

Uwanja wa Benjamin Mkapa unatoa faida kubwa kwa Simba, hasa kutokana na uwepo wa mashabiki wao, lakini pia ikibebwa zaidi na rekodi inapocheza hapo.

Rekodi zinaonyesha tangu 2018 hadi msimu huu, Simba imecheza mechi 35 za Caf na kupoteza tatu tu ilipolala 3-1 kwa Jwaneng Galaxy, ikalazwa 3-0 na Raja Casabalanca kisha ikafungwa Al Ahly 1-0. Yenyewe imeshinda michezo 25. Saba iliisha kwa sare ikifunga mabao 73 na kufungwa 19.


Kundi la Simba


        P    W    D    L    GF    GA    Pts
1.Constantine    2    2    0    0    3    1    6
2.Simba        2    1    0    1    2    2    3
3.Bravos    2    1    0    1    3    3    3
4.Sfaxien    2    0    0    2    2    4    0


Matokeo & ratiba ya Simba

Novemba 27, 2024
Simba 1–0 Bravos

Desemba 8, 2024
CS Constantine 2–1 Simba

Desemba 15, 2024
Simba v CS Sfaxien

Januari 5, 2025
CS Sfaxien v Simba

Januari 12, 2025
Bravos v Simba

Januari 19, 2025
Simba v CS Constantine