Marhathon kusaidia Watoto wachanga waliokosa malezi

Diwani wa kata ya Kisarawe ii Issa Zahoro akizindua mbio za hisani za Taasisi ya Jerusalem kwa kumvisha medali mmoja wa wakimbiaji.
Muktasari:
- Taasisi ya Jerusalem Children Home imezindua mbio za hisani zitakazofanyika Julai 19, 2025, kuchangisha fedha za kusaidia malezi ya watoto waliokosa familia kutokana na maradhi, vifo na migogoro ya ndoa.
Dar es Salaam. Taasisi ya Jerusalem imeandaa mbio maalumu za hisani kwa lengo la kuchangisha fedha zitakazosaidia malezi ya watoto wachanga wanaokosa malezi kutokana na changamoto mbalimbali kama matatizo ya afya ya akili kwa wazazi, migogoro ya ndoa na maradhi.
Mbio hizo, zitakazoanza rasmi Julai 19, 2025, zitakuwa za umbali wa kilomita 5, 10 na 21, na zinalenga kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa makazi kwa watoto wachanga zaidi ya 100 waliokosa huduma za wazazi wao.
Huu ni msimu wa nne wa mbio hizo, zikiwa na kaulimbiu "Step to Reality" (Hatua Kuelekea Uhalisia).
Akizungumza leo Aprili 27, 2025 wakati wa uzinduzi wa mbio hizo, Diwani wa Kata ya Kisarawe II, Issa Zahoro amesema tatizo la watoto kukosa malezi limechangiwa na migogoro ya ndoa pamoja na hofu ya kugawana mali.
“Watoto wa mitaani ni changamoto kubwa, wengine wanaishi katika mazingira magumu pamoja na wazazi wao. Vijana wengi wanaepuka ndoa kutokana na hofu ya kugawana mali wanapopata talaka. Hili limechangia ongezeko la watoto wasiolelewa ipasavyo,” amesema Zahoro.
Aidha, Zahoro amepongeza mbio za Jerusalem Children's Home Marathon kwa kuibua fursa ya kupata fedha za kujenga makazi na kusomesha watoto hao.
Kwa upande wake, Mwanzilishi wa Taasisi ya Jerusalem Children Home, Upendo Ngoda amesema wanatarajia kushirikisha zaidi ya watu 2,000 katika mbio hizo.

Muonekano wa jengo linalojengwa kusaidia makazi ya watoto wachanga waliokosa malezi kwa wazazi wao
Ameeleza kuwa mbio hizi ni sehemu ya jitihada za awamu ya nne za taasisi hiyo, ambayo tayari imeanza ujenzi wa nyumba kubwa itakayojumuisha hospitali na shule kwa ajili ya watoto hao.
“Hadi sasa tunalea watoto 32, na tumewasaidia zaidi ya 50. Tulianza na watoto wawili na idadi imeongezeka, hivyo tumeona umuhimu wa kuanzisha mbio hizi ili kupata rasilimali zaidi za kujenga makazi mapya,” amesema Upendo.
Ameongeza kuwa asilimia 90 ya watoto wanaopokelewa katika taasisi yao ni watoto ambao wazazi wao walikumbwa na changamoto za afya ya akili baada ya kujifungua, kuwa na maambukizi ya VVU, au kupitia migogoro ya ndoa.
Upendo amesisitiza kuwa lengo lao ni kuhakikisha watoto wote wanapata haki sawa ya elimu na malezi, na hivyo wanapanga kuanzisha hospitali na shule maalum zitakazotoa huduma ya karibu zaidi kwa watoto hao.
Mbio hizi zitafanyika Kigamboni, katika eneo la Kibada. Katibu wa Kamati ya Maandalizi ya mbio hizo, Edger Ngonyani, amesema tukio hilo sio tu kwa ajili ya kukuza afya, bali pia ni njia ya kuwawezesha watoto wasio na uwezo kupata fursa ya maisha bora baadaye.
“Tunawahamasisha watu kuonyesha upendo kwa vitendo kwa watoto, kwa kutambua kuwa kusaidia jamii ni sehemu ya kujenga maisha ya upendo kwa watoto wetu,” amesema Ngonyani.