Man United yatajiwa bei ya Jackson
Muktasari:
- Hilo linaonekana linaweza kuwa kikwazo kwa uhamisho wa wachezaji hao wawili lakini kigingi zaidi kinaonekana kuwa kwa Garnacho ambaye hana ofa nyingi mezani.
London, England. Chelsea imeripotiwa kwamba itahitaji kitita cha Pauni 80 milioni kutoka kwa Manchester United katika dirisha linaloendelea la usajili wa majira ya kiangazi ili imuachie mshambuliaji Nicolas Jackson.
Hiyo imekuja baada ya Manchester United kutajwa kuwa katika mikakati ya kuishawishi Chelsea ikubali uhamisho wa kumbadilisha Jackson na mshambuliaji wake Alejandro Garnacho.
Garnacho hayupo katika mipango ya Meneja wa Manchester United, Ruben Amorim na ikataka kumtumia kama chambo ili impate Jackson ambaye anaonekana sio sehemu ya vipaumbele vya meneja wa Chelsea, Enzo Maresca
Hata hivyo Chelsea inaamini kwamba Garnacho ana thamani chini ya Pauni 50 milioni ambayo ni ndogo kulinganisha na ile ya Jackson ambaye inaamini anaweza kuuzwa kwa Pauni 80 milioni hivyo ili mpango wa uhamisho huo kufanyika, ni Man United kuwapa Garnacho na kiasi cha fedha.
Hilo linaonekana linaweza kuwa kikwazo kwa uhamisho wa wachezaji hao wawili lakini kigingi zaidi kinaonekana kuwa kwa Garnacho ambaye hana ofa nyingi mezani.
Tangu Jackson alipojiunga na Chelsea mwaka 2023, amefunga idadi ya mabao 30 katika michezo 81 ya mashindano tofauti na kati ya hayo, mabao 24 amepachika katika Ligi Kuu ya England (EPL).
Mkataba wa Jackson na Chelsea utafikia tamati 2033 lakini kwa sasa nyota huyo wa Senegal anakabiliwa na ushindani mkali wa nafasi kutoka kwa Joao Pedro na Liam Delap walionunuliwa katika dirisha la sasa la usajili.
Kwa upande wa Garnacho, Man United inapambana kuhakikisha anaondoka ili afungue mlango wa kuingia kwa nyota mpya katika safu yake ya ushambuliaji.
Mshambuliaji huyo raia wa Argentina mwenye umri wa miaka 24, amefunga mabao 24 na kutoa pasi za mwisho 22 katika mechi 144 alizoichezea Man United.