Man City yatwaa Kombe la Carabao ikiilaza Arsenal
Wachezaji wa kikosi cha Manchester City wakishangilia Ubingwa wa Kombe la Carabao baada ya kuibuka na ushindi katika mechi ya fainali dhidi ya Arsenal, Machi 22, 2026. Picha na Mtandao
Muktasari:
- Vigogo hao wa Manchester sasa wamefikisha idadi ya mataji tisa ya Kombe hilo wakishika nafasi ya pili nyuma ya Majogoo wa Anfield, Liverpool ambao ndio vinara wakiwanayo 10.
London, England. Manchester City wamekatisha ndoto ya Arsenal ya kutwaa makombe manne msimu huu baada ya kuibuka na ushindi na kutwaa Kombe la Carabao katika fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Wembley.
City walionekana kukosa makali katika kipindi cha kwanza, lakini walirejea kwa nguvu kipindi cha pili na kufunga mabao mawili ya haraka yaliyowapa taji hilo.
Nyota wa mechi hiyo ni Nico O'Reilly, ambaye ameng’ara siku moja tu baada ya kutimiza miaka 21, akifunga mabao mawili na kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi.
Bao la kwanza lilipatikana dakika ya 60 baada ya kipa wa Arsenal, Kepa Arrizabalaga kushindwa kuudhibiti mpira wa krosi uliopigwa na Rayan Cherki, hali iliyomruhusu O’Reilly kufunga kwa kichwa.
Dakika nne baadaye, O’Reilly aliongeza bao la pili kwa kichwa kingine, akimalizia krosi iliopigwa kutoka kwa Matheus Nunes.
Kwa ushindi huo, kocha wa Man City, Pep Guardiola ameweka rekodi mpya kwa kuwa kocha wa kwanza kushinda Kombe la Carabao mara tano, akiendelea kuthibitisha ubora wake katika soka la England.
Vigogo hao wa Manchester sasa wamefikisha idadi ya mataji tisa ya Kombe hilo wakishika nafasi ya pili nyuma ya Majogoo wa Anfield, Liverpool ambao ndio vinara wakiwanayo 10.