Makocha 10 watajwa Spurs ikimtimua Postecoglou

Muktasari:
- Postecoglou alijiunga na Tottenham Hotspurs mwaka 2023 na mafanikio makubwa kwake ni kuipa ubingwa wa Europa League msimu wa 2024/2025.
Tottenham Hotspur inahusishwa na makocha 10 ambao mmojawapo anaweza kurithi mikoba ya Ange Postecoglou aliyetimuliwa leo Ijumaa, Juni 6, 2025.
Licha ya kuipa Spurs ubingwa wa Europa League msimu wa 2024/2025, Postecoglou ameonekana kushindwa kuishawishi timu hiyo kuendelea naye na leo imeamua kumuonyesha mlango wa kutokea.
Uongozi wa Spurs umeonyesha kutofurahishwa na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika Ligi Kuu England msimu uliomalizika ambapo imemaliza ikiwa nafasi ya 17 kwenye msimamo.
"Pamoja na kwamba kushinda Europa League msimu huu ni moja ya nyakati kubwa za klabu, hatuwezi kuegemeza uamuzi wetu kwenye hisia zinazolingana na ushindi huu.
"Ni muhimu kuweza kushindana katika nyanja nyingi na tunaamini mabadiliko ya mbinu yatatupa nafasi nzuri zaidi kwa msimu ujao na zaidi.
"Hili limekuwa moja ya maamuzi magumu ambayo tumelazimika kufanya na sio uamuzi ambao tumeuchukua kwa urahisi, wala ambao tumeharakisha kuhitimisha.
'Tumefanya kile tunachoamini kuwa ni uamuzi sahihi wa kutupa nafasi nzuri ya mafanikio ya kusonga mbele, sio uamuzi rahisi,” imefafanua taarifa ya Spurs.
Na baada ya kumtimua Postecoglou, Spurs ina orodha ya makocha 10 mkononi ambao inaweza kumchukua mmojawapo.
Kocha wa Brentford, Thomas Frank anaongoza orodha hiyo na anapewa nafasi kubwa kutokana na kile alichokifanya ndani ya miaka sita aliyoitumikia Brentford.
Makocha wengine ni Andoni Iraola (Bournemouth), Oliver Glasner (Crystal Palace), Marco Silva (Fulham), Roberto de Zerbi (Marseille), Mauricio Pochettino (timu ya taifa ya Marekani), Edin Terzic, Francesco Farioli, Kieran McKenna (Ipswch), Gareth Southgate na Xavi