Maajabu 10 ya Ivory Coast Afcon 2023

Muktasari:
- Mabao ya kiungo, Franck Kessie kwa mikwaju ya penalti yaliiwezesha Ivory Coast kuiondosha Senegal na kutinga hatua ya robo fainali za Afcon 2023.
Dar es Salaam. Wenyeji wa fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, Ivory Coast wameushangaza ulimwengu wa soka baada ya kufanikiwa kuwaondoa mabingwa watetezi Senegal kwa mikwaju ya penalti na kutinga robo fainali.
Bao la kusawazisha dakika za lala salama la kiungo, Franck Kessie liliirudishia matumaini Ivory Coast ya kuendelea kusalia kwenye mashindano hayo baada ya mshambuliaji, Habib Diallo kuifungia Senegal bao dakika ya nne katika mchezo huo.
Dondoo
- Ivory Coast ilitinga hatua ya 16 bora akiwa ‘best looser’ baada kumaliza nafasi ya tatu kwenye kundi A.
- Matumaini ya Ivory Coast yalififia zaidi baada ya kupokea kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Equitorial Guinea.
- ‘The Ivorian’ imeiondosha Senegal ambayo ndio mabingwa watetesi wa Afcon.
- Kiungo Franck Kessie aliyebeba matumaini ya Ivory Coast aliingia dakika ya 75 akichukua nafasi ya Ibrahim Sangare.
- Kessi alifunga mabao mawili yaliyofufua matumaini kwa timu yake bao la kusawazisha na penalti ya mwisho.
- ‘The Elephants’ ilimiliki mpira zaidi ya asilimia 50 kipindi chote cha pili na kuwazidi Senegal vitu vingi uwanjani.
- Ivory Coast ilipiga pasi za kufika 577 katika mchezo huo huku Senegal akipiga 435.
- The Elephants ilitengeneza mashambulizi ya hatari 56 huku Senegal ikitengeneza 40.
- Mashuti yaliyolenga goli kati mchezo huo Ivory Coast ilipiga manne na Senegal matatu.
- Mpaka hatua iliyofikia Ivory Coast imefanikiwa kushinda mchezo mmoja tu dhidi ya Guinea Bissau.
Ivory Coast imetangulia robo fainali itakayochezwa Jumamosi Februari 3, mwaka huu na inasubiri mshindi kati ya Mali au Burkina Faso ambao watacheza mechi yao ya hatua ya 16 bora katika Jiji la Korhogo.