Vita yabaki kwa Aziz KI, Diarra

Baada ya Taifa Stars kutolewa kwenye michuano ya Afcon 2023, sasa vita imehamia hatua ya 16 Bora kwa mastaa wawili, Djigui Diarra anayeichezea Mali na kiungo Stephen Aziz Ki raia wa Burkina Faso.
Ratiba iliyotolewa na Caf juzi usiku inaonyesha kuwa Mali itavaana na Burkina Faso kwenye mchezo wa hatua ya 16 Bora,ikiwa ni vita kati ya mastaa hao wawili wa Yanga ambao wakiwa hapa nchini wanapambana kuhakikisha timu yao inapata ushindi, lakini kule Ivory Coast kila mtu atakuwa anamuombea mwenzie mabaya.
Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Januari 30 kuanzia saa 2:00, katika Uwanja wa Amadou Gon Coulibaly, mechi hii itawagawa mashabiki wa soka hapa nchini kutokana na mapenzi yao kwa mastaa hao ambao msimu huu wamefanya vizuri, Diarra ameichezea Yanga dakika 810, huku Aziz Ki akicheza 875.
Aziz Ki amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha Burkina Faso kwenye fainali hizi akiwa amecheza michezo yote ya Afcon ya hatua ya makundi, sawa na Diarra ambaye amepata nafasi ya kuanza kwenye kila mchezo pamoja na kwamba kabla ya fainali hizi hakuwa chaguo la kwanza.
Mshindi wa mchezo huo, atafuzu hatua ya robo fainali ambapo atavaana na mshindi kati ya bingwa mtetezi Senegal na Ivory Coast mchezo utakaopigwa Januari 29, saa 5:00 usiku.
Hii ina maana kuwa Yanga ndiyo timu pekee hapa nchini hadi sasa kuwa na uhakika wa staa wake mmoja kucheza hatua ya robo fainali ya Afcon mwaka huu nchini Ivory Coast na kuweka rekodi mpya.
Mbali na hao, mashabiki wa Simba kwa sasa watakuwa wakiiunga mkono DR Congo ambayo anaitumikia beki wao Henock Inonga ambaye ameanza kwenye michezo miwili kati ya mitatu ya hatua ya makundi.
Congo ambayo ilikuwa kundi moja na Taifa Stars ilifuzu hatua ya 16 Bora ikiwa mshindi wa pili wa kundi na sasa itavaana na Misri, Januari 28 saa 5:00.
Endapo Congo itafuzu hatua hiyo mbele ya Misri, itakwenda robo fainali kukutana na mshindi wa mchezo wa majirani kati ya Guinea ya Ikweta dhidi ya Guinea Bissau mechi ambayo itapigwa Januari 28 saa 2:00, usiku.
Mechi zingine za hatua hiyo ni pamoja na Angola dhidi ya Namibia Januari 27 saa 2:00 usiku, kisha saa 5:00 Nigeria itapambana na Cameroon.
Cape Verde itakutana na Mauritania Januari 29 saa 2:00, huku Morocco ikivaana na Afrika Kusini, Januari 30 saa 5 :00 usiku.
Ratiba kamili:
Jan 27: Angola vs Namibia.
Jan 27: Nigeria vs Cameroon.
Jan 28: Equatorial Guinea vs Guinea.
Jan 28: Misri vs DR Congo.
Jan 29: Cape Verde vs Mauritania.
Jan 29: Senegal vs Ivory Coast.
Jan 30: Mali vs Burkina Faso.
Jan 30: Morocco vs Afrika Kusini