Liverpool yamaliza ukame wa ushindi, Salah mambo magumu
Muktasari:
- Baada ya kuanza msimu kwa kasi kwa kushinda mechi saba mfululizo katika michuano yote, Liverpool ilipoteza mwelekeo kwa kufungwa mechi nne mfululizo, ikiwemo dhidi ya mahasimu wao Manchester United kwenye Ligi Kuu siku ya Jumapili.
Liverpool imekomesha mwenendo wao mbaya wa kupoteza mechi kwa kishindo, baada ya kutoka nyuma na kuicharaza Eintracht Frankfurt katika Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku wa Oktoba 22, 2025.
Baada ya kuanza msimu kwa kasi kwa kushinda mechi saba mfululizo katika michuano yote, Liverpool ilipoteza mwelekeo kwa kufungwa mechi nne mfululizo, ikiwemo dhidi ya mahasimu wao Manchester United kwenye Ligi Kuu siku ya Jumapili.
Awali, ilionekana kama hali hiyo mbaya ingeendelea baada ya kuruhusu kutanguliwa kwa bao moja nchini Ujerumani lililofungwa na beki wa zamani wa Leeds, Rasmus Kristensen.
Hata hivyo, Liverpool iligeuza matokeo baada ya Ekitike kufunga bao la kusawazisha dakika ya 35 kabla ya beki Virgil van Dijk na Ibrahima Konate kufunga mabao mengine mawili kabla ya mapumziko.
Liverpool iliendelea kutafuta ushindi kwa kuongeza mabao mawili katika kipindi cha pili. Cody Gakpo alifunga bao lake la nne msimu huu kwa kumalizia pasi ya Florian Wirtz, kabla ya Dominik Szoboszlai kufunga shuti kali la mbali lililokamilisha ushindi huo mnono kwenye Uwanja wa Deutsche Bank Park, Ujerumani.
Salah mambo magumu
Salah alianza mechi hiyo akiwa benchi, huku kocha Arne Slot akimpa nafasi dakika ya 74 wakati Liverpool ikiwa tayari inaongoza kwa mabao 5-1.
Dakika za mwisho za mchezo, Salah alipata nafasi nzuri ya kumpasia Wirtz ambaye bado hajafunga tangu ajiunge na Liverpool kwa dau nono la pauni milioni 116 akitokea Bayer Leverkusen, lakini badala yake akaamua kupiga mwenyewe jambo lililowakera mashabiki.
Salah alikuwa kwenye kiwango cha juu msimu uliopita, akifunga magoli 34 na kutoa pasi 23 za mabao katika michezo 52, na hata kutunukiwa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka wa PFA, lakini safari hii mambo si mazuri amefunga magoli matatu pekee na kutoa asisti tatu kwenye mechi 12 za msimu huu.