Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwaheri Mwinyi, Kwaheri mwanamichezo

Muktasari:

  • Mzee Mwinyi ambaye amewahi pia kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya mapafu na kwa mujibu wa ratiba ya msiba iliyotolewa na serikali, mazishi yake yatafanyika leo Jumamosi, Visiwani Zanzibar.

Dar es Salaam. Jana Alhamisi, Februari 29, Taifa lilipata habari mbaya ya msiba wa aliyekuwa Rais wa awamu ya pili wa Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi aliyefariki katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Emilio Mzena saa 11:30 jioni wakati akipatiwa matibabu.

Mzee Mwinyi ambaye amewahi pia kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya mapafu na kwa mujibu wa ratiba ya msiba iliyotolewa na serikali, mazishi yake yatafanyika leo Jumamosi, Visiwani Zanzibar.

Kifo cha Rais Mwinyi kimetokea ikiwa haujatimia hata mwezi mmoja tangu Tanzania impoteze aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ambaye alifariki Februari 10 jijini Dar es Salaam na kuzikwa Februari 17, huko Monduli.

Hayati Rais Mwinyi atakumbukwa kwa mengi aliyoyafanya na mafanikio ya sekta mbalimbali yaliyopatikana wakati wa utawala wake ambao ulidumu kuanzia 1985 hadi 1995.

Wadau wa sekta ya michezo ni miongoni mwa makundi ambayo yatamkumbuka sana Rais Mwinyi kutokana na ushiriki wake wa mara kwa mara katika shughuli mbalimbali za kimichezo lakini pia namna ambavyo utawala wake uliipa kipaumbele jambo lililopelekea kupatikana kwa mafanikio mengi katika miaka 10 ambayo aliiongoza serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Gazeti hili linakuletea kumbukumbu mbalimbali za hayati Rais Mwinyi michezoni ambazo zinaacha alama nzuri ya namna alivyojitoa mara kwa mara kuhakikisha mafanikio ya sekta hiyo hapa Tanzania yanapatikana.

Ujenzi wa Viwanja

Utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi, ulifanya kazi kubwa kuhimiza na kusapoti ujenzi wa viwanja vya michezo hasa soka na kuendeleza vizuri kile kilichofanywa na mtangulizi wake, hayati Julius Nyerere cha kuweka mkazo katika ujenzi wa miundombinu hiyo muhimu kwa mujibu wa sheria 17 za mchezo wa soka.

Viwanja vitano vya soka ambavyo vimetumika kwa mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano mengine kwa nyakati tofauti vilijengwa wakati wa utawala wa Rais Mwinyi ambaye leo hii amelala usingizi wa mauti.

Muda mfupi tu baada ya kuingia madarakani, ilishuhudiwa uwanja wa michezo ambao ulipewa jina lake la Ali Hassan Mwinyi uliopo huko mkoani Tabora ukijengwa na leo hii unatumiwa kwa mechi za nyumbani za Tabora United wakati mwaka 1988, kulianza ujenzi wa kiwanja cha Manungu Complex ambacho kinamilikiwa na kiwanda cha sukari cha Mtibwa, Morogoro na pia kiwanja kingine kikiwa ni cha Karume kilichopo, Musoma, Mara.

Mwaka 1989, mkoani Kilimanjaro kulijengwa Uwanja wa Ushirika na mwaka 1992 ulijengwa Uwanja wa kumbukumbu ya Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Mafanikio michezoni

Utawala wa Rais Mwinyi unaweza kuwa miongoni mwa nyakati ambazo Watanzania walishudhuhudia mafanikio makubwa michezoni na hilo lilichagizwa kwa kiasi kikubwa na mapenzi ya hayati huyo kwa sekta hiyo.

Mwaka 1993, Simba iliweza kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Caf, mafanikio ambayo yalikuwa ni makubwa zaidi kufikiwa na klabu ya Tanzania katika mashindano ya klabu Afrika ingawa ilipoteza kwa mabao 2-0 mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast katika mechi ya nyumbani ambayo Hayati Mwinyi alikuwepo uwanjani, huku mechi ya ugenini wawakilishi hao wa Tanzania wakiwa wametoka sare tasa.

Simba hiyohiyo mwaka 1994, iliingia hatua ya robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika ambapo ilitolewa na Nkana ya Zambia kwa kufungwa mabao 4-3.

Katika kipindi cha utawala wa Rais Mwinyi, timu za Tanzania zilionekana kutawala mashindano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati ambayo kwa sasa yanajulikana kama Kombe la Kagame ambapo Simba ilichukua mara tatu ambazo ni mwaka 1991, 1992 na 1995 wakati Yanga ilitwaa mara moja ambayo ni mwaka 1993.

Yanga pia mwaka 1995, iliupa heshima utawala wa Rais Mwinyi baada ya kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la Washindi Afrika.

Mwaka 1994, timu ya taifa ya Tanzania Bara ilitwaa ubingwa wa mashindano ya Cecafa Chalenji na mwaka mmoja baadaye, Zanziabr ikafuata nyayo.

Mwaka 1989, mwanariadha Juma Ikangaa aliibuka mshindi wa mbio ndefu za New York Marathon kabla ya kutwaa medali za fedha mara mbili kwenye mbio nyingine kubwa ya Boston Marathon 1988 na 1990.