Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kocha aibua mpya ishu ya Che Malone, Camara

DABI Pict

Muktasari:

  • "Tuna mapumziko ya siku moja au mbili ili kupata nafuu kisha tunaanza maandalizi ya mchezo huo dhidi ya Yanga, tunajua itakuwa ni wiki ya kusisimua kwa mashabiki ambayo ni muhimu kwetu sisi kuwafurahisha,"

Arusha. Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids ameshamaliza kazi aliyioifuta jijini Arusha wakati walipoikabili Coastal Union juzi na kupata ushindi wa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, ambapo Steven Mukwala alifunga hat trick, ikiwa ni ya tatu kwa msimu huu katika Ligi Kuu Bara.

Kocha huyo anajua kibarua kilichopo mbele yake kwa sasa ni kuikabili Yanga katika pambano la Dabi ya Kariakoo litakalopigwa Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam likiwa ni pambano la pili kwa msimu huu katika Ligi Kuu na la 114 tangu katika Ligi ya Bara tangu 1965.

Katika kuwatoa hofu mashabiki wa timu hiyo, Kocha Fadlu amewahakikishia kuwa, kipa Moussa Camara na beki, Fondoh Che Malone watacheza katika Dabi hiyo.

Nyota hao wawili wa kikosi cha kwanza walikosa pambano la juzi dhidi ya Coastal Union na Simba ilishinda kwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha ikiwa ni mara ya kwanza kwa wachezaji hao kukosekana hususani kipa Camara na wote walikuwa majeruhi.

Wachezaji hao waliumia katika pambano la Dabi ya Mzizima dhidi ya Azam FC lililoisha kwa sare ya mabao 2-2.

Fadlu anaenda katika mchezo huo akiwa na mwenendo mzuri ndani ya ligi baada ya kucheza mechi 21 na kukusanya pointi 54 katika nafasi ya pili, nne tofauti na ilizonazo kinara Yanga yenye pointi 58 kutokana na mechi 22. Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Oktoba 19, 2024, Yanga ilishinda 1-0.

Kocha huyo, aliyeiwezesha Simba kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikijiandaa kuvaana na Al Masry ya Misri mapema mwezi ujao, alisema wachezaji hao hadi Jumamosi watakuwa fiti.

“Che Malone na Camara watakuwa tayari kwa Dabi, kwani tuna wiki ya kufanya maandalizi kwa ajili ya mchezo huo, lakini kila mchezaji kwa sasa anayepata nafasi anacheza vizuri,” alisema Fadlu, raia wa Afrika.

“Hata mechi iliyopita dhidi ya Coastal unaona alikaa nje Mohamed Hussein, lakini Valentin Nouma akacheza vizuri, kulia kulikuwa na David Kameta ‘Duchu’ akacheza vizuri pia Deborah Mavambo akacheza vizuri sana hivyo naweza kusema kila mchezaji anajua namna ya kutimiza wajibu wake.”

Fadlu aliongeza, kazi kubwa ambayo watafanya kama timu ni kuwa tayari kwa ajili ya mchezo wa Dabi ili kwenda pia kupata ushindi utakaoongeza morali na kutengeneza njia nyeupe ya kwenda kwenye kilele cha mafanikio ambayo ni kutwaa ubingwa wa ligi.

“Tuna mapumziko ya siku moja au mbili ili kupata nafuu kisha tunaanza maandalizi ya mchezo huo dhidi ya Yanga, tunajua itakuwa ni wiki ya kusisimua kwa mashabiki ambayo ni muhimu kwetu sisi kuwafurahisha,” alisema Fadlu.

Camara aliyetumika katika mechi 20 zilizopita za ligi ikiwa ni sawa na dakika 1,800 ameruhusu mabao manane tu akiifanya Simba kuwa timu iliyoruhusu mabao machache zaidi hadi sasa, huku mwenyewe akiwa na rekodi ya clean sheet 15, kama zilizowekwa msimu uliopita na Ley Matampi aliyekuwa Coastal.