Kichapo chamvuruga Maresca akiwaomba msamaha mashabiki Chelsea

Muktasari:
- Enzo Maresca alijiunga na Chelsea, Julai Mosi, 2024 akitokea Leicester City na mkataba wake utafikia tamati, Juni, 2029.
Kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Brighton jana, Februari 14, kimemchanganya meneja Enzo Maresca wa Chelsea ambaye amegeuka mbogo kwa wachezaji wake huku akiwaangukia mashabiki wa timu hiyo.
Mabao mawili ya Yankuba Minteh na lingine moja la Kaoru Mitoma yaliihakikishia ushindi huo mnono ambao umekuwa mchungu kwa Maresca na vijana wake.
Maresca amesema si tu wamepoteza mchezo bali pia hawakuonyesha kiwango kizuri katika dakika nyingi za mechi.
“Nawaomba radhi mashabiki. Sio kiwango kizuri ambacho tunaweza kukitoa, hasa wakati huu kwenye msimu. Tunatakiwa kusimama pamoja.
“Nahisi presha kila wakati. Kiwango kilikuwa kibaya zaidi tangu nilipowasili hivyo sio wakati sahihi lakini bado tupp nafasi ya nne na katika mbio za kumaliza Ulaya,” alisema Maresca.
Ikiwa imecheza mechi moja zaidi ya Manchester City, Newcastle United, Bournemouth na Aston Villa, Chelsea inaweza kujikuta ikiangukia katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa EPL iwapo washindani wenzake hao wa nafasi ya nne wataibuka na ushindi katika mechi zao za wikiendi hii.
Na hilo limemfanya Maresca akiri kuwa wanazidi kujiweka katika wakati mgumu katika vita ya kuwania nafasi ya nne ambayo itawahakikishia kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
“Matokeo haya, mvurugiko unahusu kila kitu. Kiukweli tunawaomba msamaha mashabiki ambao wamekuja hapa na muda huu tupo katika nafasi tuliyopo.
“Tunatakiwa kufanya vizuri zaidi ya tulivyofanya usiku. Nadhani kwa maana ya kutawala mchezo au kutunza mpira tumefanya hivyo. Lakini nimesema kabla ya mchezo unapokuwa hauna mshambuliaji ambaye anaweza kuwa tishio tunahitajika kutafuta masuluhisho tofauti. Sio suala la nafasi,” alisema Maresca.
Meneja huyo alisisitiza kuwa Chelsea inapaswa kuvalia njuga mechi zilizobakia ili iweze kutimiza malengo yake.
“Kuna mambo mengi tunatakiwa kufanya vizuri. Tuna mechi nyingi na tupo katika nafasi nzuri. Tunatakiwa kufanya kile tunachoweza na kujaribu kumaliza katika njia bora.
“Tupo katika nyakati ambayo tunahisi tunaweza kufungwa bao kirahisi na tukahangaika kufunga. Nadhani kabla ya goli hawakuwa na nafasi. Kuna mengi ambayo tunatakiwa kuyafanya vyema,” alisema Maresca.