Chelsea: Hatutaki ubingwa

Muktasari:
- Kwa sasa, Liverpool ina pointi 36, Chelsea in pointi 34, Arsenal imekusanya pointi 30 na Manchester City yenyewe ina pointi 27.
London, England. Meneja wa Chelsea, Enzo Maresca amesema kuwa timu yake haipo tayari kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu England (EPL) licha ya muendelezo wa matokeo mazuri ambao wamekuwa nayo katika siku za hivi karibuni.
Ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Brentford juzi Jumapili ulikuwa wa saba mfululizo kwa Chelsea katika mechi za mashindano tofauti inayoshiriki msimu huu huku ukiifanya izidi kujiimarisha katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa EPL.
Matokeo hayo yaliifanya Chelsea kupunguza pengo la pointi baina yake na kinara Liverpool kubakia mbili huku ikiitangulia Arsenal iliyopo katika nafasi ya tatu kwa pointi nne na iko mbele ya bingwa mtetezi Manchester City kwa pointi saba.
Kwa sasa, Liverpool ina pointi 36, Chelsea in pointi 34, Arsenal imekusanya pointi 30 na Manchester City yenyewe ina pointi 27.
Hata hivyo pamoja na timu yake kuwa katika muelekeo mzuri katika mbio za kuwania ubingwa EPL msimu huu, kocha Maresca amewataka mashabiki wa timu yake na wadau wa soka kutoipa Chelsea imani ya kutwaa ubingwa wa ligi ya England msimu huu.
"Sio suala la mechi ngapi umeshinda, ni jambo la kuwa na uhalisia. Kuna mambo tunatakiwa kufanya vizuri. Na ndio maana nasema kwa kwangu mimi, hatupo tayari," alisema Maresca.
Makali ya safu ya ushambuliaji yanaonekana kuwa silaha kubwa kwa Chelsea katika siku za hivi karibuni ambapo imeonyesha uwezo mkubwa wa kufumania nyavu na kutengeneza mashambulizi kulinganisha na timu nyingine.
Hadi sasa, Chelsea ndio kinara wa kufunga mabao katika EPL msimu huu ambapo hadi sasa imeshafunga mabao 37 ikifuatiwa na Liverpool iliyo na mabao 31, Arsenal ina mabao 29 na Manchester City imefumania nyavu mara 28.
Timu hiyo pia inashika nafasi ya pili kwa kupiga idadi kubwa ya mashuti hadi sasa ikiwa nayo 256 huku kinara ikiwa ni Manchester City ambayo uina mashuti 282, Liverpool imepiga mashuti 232 na Arsenal ina mashuti 226.
Katika mchezo dhidi ya Brentford juzi, mabao ya Chelsea yalifungwa na Marc Cucurella na Nicolas Jackson huku moja la kufutia machozi la wapinzani wao likifungwa na Bryan Mbeumo.
Tangu ilipofungwa na Newcastle United kwa mabao 2-0 katika mechi ya Ligi Kuu England, Oktoba 30 mwaka huu, Chelsea haijapoteza mechi 10 mfululizo za mashindano tofauti, ikishinda michezo nane na kutoka sare mbili.
Katika mechi hizo 10 mfululizo ambazo Chelsea haijapoteza kwenye mashindano mbali inayoshiriki, imefunga mabao 31 ikiwa ni wstani wa mabao 3.1 kwa mchezo huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara tisa ikiwa ni wsstani wa bao 0.9 kwa mechi.
Makali ya timu hiyo hayaishii kwenye EPL pekee kwani hata katika mashindano ya Uefa Conference League imekuwea moto wa kuotea ambali ambapo kwa sasa inaongoza msimamo ikiwa imekusanya pointi 15 katika mechi tano hivyo kujiweka katika mazingira mazuri ya kuingia hatua inayofuata.