Kipigo cha Man City kilivyoipa rekodi United

Muktasari:
- Ruben Amorim kocha wa Manchester United anafanikiwa kuifunga Manchester City ya Pep Guardiola mara mbili mfululizo ambapo mara ya kwanza aliifunga kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mabao 4-1 alipokuwa Sporting CP ya Ureno.
Manchester United imefanikiwa kupata ushindi hapo jana dhidi ya Manchester City katika mchezo wa Ligi Kuu England ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Etihad.
Man City ilikuwa ya kwanza kupata bao ambalo lilifungwa na Joško Gvardiol dakika ya 36, mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika City iliondoka ikiwa inaongoza.
Kipindi cha pili kilianza ambapo Man City iliendelea kuongoza mpaka dakika ya 88 ambapo Bruno Fernandez aliifungia bao Man United kwa mkwaju wa penalti baada ya Amad Diallo kuchezewa vibaya kwenye eneo la hatari na beki wa Man City Matheus Nunes.
Dakika ya 90 United ilipata bao la pili kupitia kwa Amad Diallo ambaye ameingia kwenye rekodi ya kuwa mchezaji wa pili wa United mwenye umri mdogo kufunga bao la ushindi dakika ya 90 dhidi ya bingwa mtetezi akiwa na miaka 22 na siku 157 ambapo mchezaji mwingine kufanya hivyo alikuwa ni Neil Mellor ambaye aliifunga Arsenal mwaka 2004.
Bao la penalti alilofunga Bruno Fernandez linakuwa bao lake la 21 katika mikwaju 25 ya penalti aliyopiga akiwa na Man United kwenye Ligi Kuu ya England akimpita nyota wa zamani wa timu hiyo Wayne Rooney mwenye mabao ya penalti 20 katika mikwaju 28 aliyopiga akiwa na timu hiyo.
Baada ya kipigo dhidi ya Manchester United, Man City imesalia na pointi 27 ikiwa nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England huku Man United ikisogea kutoka nafasi ya 14 mpaka nafasi ya 13 ikiwa na pointi 22 katika michezo 16 iliyocheza.
Ruben Amorim kocha wa Manchester United anafanikiwa kuifunga Manchester City ya Pep Guardiola mara mbili mfululizo ambapo mara ya kwanza aliifunga kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mabao 4-1 alipokuwa Sporting CP ya Ureno. Ushindi wa United unakuwa wa pili kwa Amorim kwenye Ligi Kuu England tangu alipojiunga na wababe hao wa Manchester.
Matokeo ya mechi nyingine
Chelsea 2 vs 1 Brentford
Southampton 0 vs 5 Tottenham
Man City 1 vs 2 Man United
Brighton 1 vs 3 Crystal Palace