Haya hapa majiji, miji misafi zaidi Tanzania

Muktasari:
- Vigezo muhimu vilivyohakikiwa ni udhibiti wa taka ngumu, upatikanaji wa maji safi na salama, udhibiti wa maji taka, matumizi ya vyoo bora, usafi katika masoko, machinjio, shule za msingi, sekondari, hospitali za halmashauri, benki na upendezeshaji wa mji, mitaa na maeneo ya maziko.
Dar es Salaam. Halmashauri ya jiji la Tanga, imetajwa kuongoza kwa usafi kwa kupata asilimia 83.2 ya alama zote. Ikishindanishwa na halmashauri sita za majiji zilizopo nchini.
Hayo yamebainishwa kwenye kilele cha Wiki ya Afya, wakati yakisomwa matokeo ya mashindano ya afya na usafi wa mazingira kwa kila kundi yaliyopatikana kutokana na uhakiki uliotumia orodha hakiki mahususi kwa kila kundi.
Taarifa iliyotolewa kwa umma leo Jumatano, Aprili 9, 2025 na Wizara ya Afya imeonyesha mashindano ngazi ya halmashauri za majiji yaliyohusisha jumla ya majiji sita ambapo Jiji la Tanga limeibuka kuwa mshindi wa kwanza kwa kupata asilimia 83.2 ya alama zote.
Ilifuatiwa na halmashauri ya Jiji la Mbeya ambalo limepata asilimia 81.5. Halmashauri ya Jiji la Arusha imekuwa ya tatu kwa kupata asilimia 80.0 ya alama zote.
Majiji yaliyoshika nafasi za mwisho ni pamoja na Jiji la Mwanza lililopata asilimia 79.2, Dar es Salaam asilimia 71.2 na Jiji la Dodoma lililopata asilimia 70.8
Vigezo muhimu vilivyohakikiwa ni udhibiti wa taka ngumu, upatikanaji wa maji safi na salama, udhibiti wa maji taka, matumizi ya vyoo bora, usafi katika masoko, machinjio, shule za Msingi, shule za sekondari, hospitali za halmashauri, benki na upendezeshaji wa mji, mitaa na maeneo ya maziko.
Katika ngazi ya halmashauri za Manispaa yaliyohusisha jumla ya Manispaa 20, halmashauri ya Manispaa ya Moshi imeibuka kuwa mshindi wa kwanza kwa kupata asilimia 84.2 ya alama zote, ikifuatiwa na Shinyanga ambayo imepata asilimia 78.0. huku ya Iringa ikiwa ya tatu kwa kupata asilimia 77.7 ya alama zote.
Ngazi ya halmashauri za miji yalihusisha jumla ya miji 21 ambapo halmashauri ya Mji wa Njombe umekua mshindi wa kwanza kwa kupata asilimia 84.4 ya alama zote, Makambako umepata asilimia 78.5. halmashauri ya Mji wa Mafinga imekuwa ya tatu kwa kupata asilimia 77.6 ya alama zote.
Ngazi ya Halmashauri ya wilaya yalihusisha jumla ya halmashauri 137 ambapo halmashauri ya Wilaya ya Njombe imeibuka kuwa mshindi wa kwanza kwa kupata asilimia 94.4 ya alama zote, ikifuatiwa na Iringa ambayo imepata asilimia 93.3. Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi imekuwa ya tatu kwa kupata asilimia 89.6 ya alama zote.
Ngazi ya mitaa, ilihusisha jumla ya mitaa 94 ambayo inapatikana katika majiji sita, Manispaa 20 na miji 21. Shughuli hiyo ilihusisha kukagua mazingira ya ujumla ambapo Mtaa wa Rengua uliopo kata ya Mawenzi, Manispaa ya Moshi, umeibuka kuwa mshindi wa kwanza.
Mawenzi imepata asilimia 90.3 ya alama zote, ikifuatiwa na Mtaa wa Nazareth uliopo kata ya Mji Mwema halmashauri ya Mji wa Njombe ulioshika nafasi ya pili ukiwa umepata asilimia 88.4 ya alama zote na mshindi wa tatu ni Mtaa wa Sido uliopo katika Kata ya Njombe Mjini, Halmashauri ya Mji Njombe uliopata asilimia 87.4 ya alama zote.
Jumla ya halmashauri za vijiji 274 zilishiriki katika mashindano kwa mwaka 2024 kwa kuzingatia vigezo ambavyo ni muhimu katika usafi wa kaya na sehemu mbalimbali za jumuiya katika kijiji.
Vigezo hivyo ni uwepo usimamizi wa mpango wa usafi wa mazingira na usambazaji endelevu wa maji vijijini, uwepo wa vyoo bora na vifaa vya kunawia mikono, udhibiti wa hali ya kujisaidia ovyo na usafi kwa ujumla katika jamii.
Mshindi wa kwanza katika kundi hili ni Kijiji cha Ikuna kilichopo Kata ya Ikuna, halmashauri ya Wilaya ya Njombe kilichopata asilimia 98.3 ya alama zote kikifuatiwa na Kijiji cha Kidegembye kilichopo Kata ya Kidegembye, halmashauri ya Wilaya ya Njombe kilichopata asilimia 96.1 ya alama zote. Nafasi ya tatu imechukuliwa na Kijiji cha Mawala kilichopo Kata ya Irole, Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kilichopata asilimia 93.9 ya alama zote.