KenGold yaahidi kurudi kwa kishindo Ligi Kuu

Muktasari:
- KenGold, iliyopanda daraja msimu huu baada ya kushika nafasi ya kwanza katika Ligi ya Championship msimu uliopita ikifuatiwan na Pamba Jiji inayoendelea kupambana kusalia kwa msimu ujao wa Ligi Kuu, imekusanya pointi 16 tu katika mechi 28
Mbeya. Pamoja na kukubali kushuka daraja, Kocha Mkuu wa KenGold Omary Kapilima amesema wanafanya kila linalowezekana kuwashawishi mastaa waliofanya vizuri kikosini ili wabaki nao kwa ajili ya kupambana katika Ligi ya Championship kwa lengo la kurudi upya katika Ligi Kuu Bara.
KenGold imeshuka daraja baada ya kushiriki Ligi Kuu msimu mmoja na sasa wanatarajia kucheza Championship msimu ujao, huku matarajio ikiwa ni kupanda tena kuungana na wengine wakiwamo Yanga na Simba.

Katika kikosi cha timu hiyo, asilimia kubwa ya wachezaji mikataba yao inaisha mwisho wa msimu huu, wakiwamo mastaa waliotua dirisha dogo kama Benard Morrison, Seleman Rashid 'Bwenzi', Obrey Chirwa, Kelvin Yondani, Zawadi Mauya, Sadala Lipangile na Kyala Lasa.

Akizungumza na Mwananchi, Kapilima alisema bado ni mapema kujua iwapo atabaki au kung’atuka baada ya ligi kuisha, akieleza kuwa kwa sasa wanasubiri kuhitimisha msimu ili kujua hatma yake.
Beki huyo wa kulia wa zamani wa Majimaji, Yanga, Mtibwa Sugar na Taifa Stars, alisema iwapo ataendelea kubaki kikosini humo, hatua ya kwanza ni kukutana na uongozi kujadiliana namna ya kuwabakiza nyota waliofanya vizuri kuwashawishi kuitumia timu hiyo ili irejee Ligi Kuu.
“Kwa kuwa tunazo mechi mbili ni ngumu kujua kama nitabaki au kuondoka, lakini iwapo nitaendelea kuwapo nitazungumza na mabosi kushawishi waliofanya vizuri waendelee kubaki ili turudi haraka Ligi Kuu,” alisema Kapilima.
Kocha huyo, aliongeza kuwa sababu ni nyingi zilizoishusha timu hiyo Championship akifafanua katika sehemu ya ufundi, beki haikuwa bora kwa kuwa kila mechi walizocheza ni takribani zote wameruhusu bao.
Alisema, kwa sasa wanakubaliana na matokeo waliyovuna, ambapo hesabu zao ni kusubili mechi mbili zilizobaki kutafuta heshima na kujiandaa upya na msimu ujao wa Championship.
“Tunakubalia na matokeo, tunasubiri kuhitimisha ligi kwa kutafuta ushindi ili kuweka heshima tu, vinginevyo tunaenda kufanya tathimini kujipanga upya na Championship msimu ujao,” alisema kocha huyo.

KenGold, iliyopanda daraja msimu huu baada ya kushika nafasi ya kwanza katika Ligi ya Championship msimu uliopita ikifuatiwan na Pamba Jiji inayoendelea kupambana kusalia kwa msimu ujao wa Ligi Kuu, imekusanya pointi 16 tu katika mechi 28.
Katika mechi hizo 28, Wachimba Dhahabu hao wameshinda tatu tu, kutoka sare saba na kupoteza 18, huku ikifunga mabao 22 na kufungwa 52 ikiwa ya pili nyuma ya Fountain Gate iliyofungwa mabao 54, lakini ikiwa ni timu ya kwanza kushuka daraja mapema, kabla ya juzi Kagera Sugar kuifuata baada ya Pamba Jiji kupata ushindi 2-0 dhidi ya KeGold na yenyewe kupoteza 1-0 nyumbani kwa Mashujaa.