Kante mlangoni kwa Simba, dili lake liko hivi
Muktasari:
- Hadi sasa ni mchezaji mmoja tu mgeni ndiye amefanikiwa kujiunga na Simba msimu huu ambaye ni beki wa kushoto kutoka Al Hilal, Khadim Diaw ambaye alitua nchini jana.
Simba imefikia makubaliano ya kumsajili kiungo raia wa Senegal, Alassane Kante kutoka timu ya Athlétique Bizertin ya Tunisia. Simba ipo kwenye harakati za kuboresha kikosi chake baada ya kuondokewa na mastaa sita kuanzia dirisha hili la usajili limefunguliwa Julai Mosi mwaka huu.
Mastaa ambao wameshaondoka Simba ni, Fernandes Mavambo, Kelvin Kijili, Fabrice Ngoma, Hussein Kazi, Aishi Manula na Valentin Nouma.
Kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids ndiye anayesimamia usajili huo na inaelezwa kuwa tayari mchezaji huyo amekubali kusaini kandarasi ya miaka miwili ndani ya Wekundu wa Msimbazi huku taarifa kutoka Tunisia zikisema kuwa leo Jumanne utapigwa mchezo maalumu wa kumuaga staa huyo.
Kante mwenye umri wa miaka 24 msimu uliopita wa 2024/2025, alihusika kwenye mabao manne katika Ligi Kuu ya Tunisia maarufu kama Ligue Pro akifunga bao moja na kutoa pasi tatu za mabao katika mechi 25 alizocheza.
Tangu ajiunge na CA Bizertin mwaka 2022, akitokea Klabu ya US Gorée ya nchini kwao Senegal, Kante amecheza mechi 72 akifunga mabao manne na kutoa pasi sita za mabao huku akionyeshwa jumla ya kadi 12 za njano.
Mchezaji huyo ambaye anatajwa kuwa mmoja kati ya viungo wa kisasa, mbali na kucheza nafasi ya kiungo mkabaji pia mchezaji huyu anaweza kutumika kama beki wa kati, sehemu ambayo tayari Simba inakaribia kumuuza beki wake, Che Malone Fondoh.
Kitendo cha kumsajili kiungo huyo ni kwenda kuziba pengo la Fabrice Ngoma ambaye alitangaza kuachana na timu hiyo mwanzoni tu mwa mwezi huu baada ya kutumika kwenye timu hiyo kwa miaka mitatu.
Ukiachana na Alassane Kante wapo wachezaji wengine ambao Simba inafukuzia kuwapata katika dirisha hili la usajili.
Mofossé Karidioula
Huyu ni winga wa kulia aliyekuwa anakipiga katika Klabu ya Harras El Hodoud ya Misri, kwa sasa mchezaji huyu yupo huru baada ya mkataba wake na timu hiyo kumalizika Julai Mosi mwaka huu.
Mpaka sasa Simba ndiyo wapo mstari wa mbele katika kuiwania saini ya winga huyo wa zamani wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
Msimu uliopita, Karidioula alicheza jumla ya mechi 15 za Ligi Kuu nchini Misri ambapo alihusika katika mabao mawili akifunga moja na kutoa pasi moja ya bao katika dakika 943 alizoicheza.
Karidioula pia amewahi kucheza Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika. Alicheza jumla ya mechi 32 ambapo 17 alizicheza katika Ligi ya Mabingwa na 15 katika Kombe la Shirikisho zote akiwa na ASEC Mimosas.
Alihusika katika mabao manne kwenye Ligi ya Mabingwa akifunga mawili na kutoa pasi mbili za mabao wakati kwenye Kombe la Shirikisho alifunga mabao matatu na kutoa pasi moja ya bao.
Hadi sasa ni mchezaji mmoja tu mgeni ndiye amefanikiwa kujiunga na Simba msimu huu ambaye ni beki wa kushoto kutoka Al Hilal, Khadim Diaw ambaye alitua nchini jana.