Kane anamaliza gundu la makombe

Muktasari:
- Kane ndiye mfungaji bora wa Bundesliga msimu huu akiwa na mabao 24 akiikimbizia rekodi yake ya msimu uliopita ambapo alifunga mabao 36.
Munich, Ujerumani. Mshambuliaji wa Bayern Munich, Harry Kane, anakaribia kumaliza msimu akiwa na kombe lakini huenda asiwe uwanjani siku ambayo timu yake itapata taji.
Kane alionyeshwa kadi ya njano wiki iliyopita katika mchezo dhidi ya Mainz, Jumamosi na hiyo itamfanya kuukosa mchezo ujao dhidi ya RB Leipzig.
Mechi hiyo, dhidi ya RB Leipzig ugenini, inaweza kuwa ya kutangaza ubingwa wa Bundesliga kwa Bayern ambao walipoteza taji hilo msimu uliopita mbele ya Bayer Leverkusen.
Bayern inahitaji ushindi tu dhidi ya Leipzig ili kutangazwa kuwa mabingwa wapya wa ligi hiyo huku bado wakiwa na mechi mbili mkononi.

Kane ndiye mfungaji bora wa Bundesliga msimu huu akiwa na mabao 24 akiikimbizia rekodi yake ya msimu uliopita ambapo alifunga mabao 36.
Staa huyu wa kimataifa wa England ni miongoni mwa washambuliaji hatari barani Ulaya lakini hadi sasa hajashinda taji lolote kubwa huku umri ukiwa unaenda kumtupa mkono.
Kucheza mchezo ambao ungeamua hatma ya ubingwa wa Bayern ilikuwa ni moja kati ya ndoto za fundi huyu lakini sasa atalazimika kutazama wenzake akiwa jukwaani.