Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kally Ongala aondolewa KMC, sababu zatajwa

Muktasari:

  • KMC inashika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na pointi 30 ilizozikusanya katika mechi 26 ambapo imeibuka na ushindi katika mechi nane, imetoka sare sita na kupoteza mechi 12.

Timu ya KMC ya Kinondoni, Dar es Salaam imeamua kuachana na kocha wake Kally Ongala kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Uamuzi huo umefanyika baada ya kocha huyo kuitumikia timu hiyo kwa miezi mitano na siku 21 tu tangu alipochukua mikoba ya Abdi Hamid Moalin ambaye aliachana na timu hiyo na kujiunga na Yanga.

Mmoja wa viongozi wa KMC amesema kuwa sababu ya kuachana na Kally Ongala ni timu hiyo kutokuwa na muendelezo wa matokeo mazuri chini yake tangu alipojiunga nayo pamoja na kiwango kisichoridhsha,

"Ni kweli tumeamua kuvunja mkataba wa kocha Ongala na sababu ni mwenendo usiorisha wa timu kwa maana ya matokeo lakini pia hata namna inavyocheza ni vibaya jambo linalosababisha ipoteze pointi kirahisi kwenye mechi nyingi," amefichua kiongozi huyo.

Katika kipindi cha miezi mitano aliyosimamia benchi la ufundi la KMC, timu hiyo imecheza mechi 15 za Ligi Kuu ambapo imekusanya pointi 16 tu jambo lililochangia kwa kiasi kikubwa iwe katika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu msimu huu.

KMC katika mechi hizo ambazo imesimamiwa na Ongala kwenye Ligi Kuu, imeibuka na ushindi ara nne, imetoka sare nne na imepoteza mechi saba huku ikifumania nyavu mara 13 na kufungwa mabao 23.

Timu hiyo pia iliondolewa katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB baada ya kufungwa bao 1-0 na Singida Black Stars.

Ongala alizaliwa London, England Agosti 31, 1979 lakini baada ya hapo makuzi na malezi yake aliyapatia jijini Dar es Salaam.

Baba yake ni Marehemu Ramadhan Mtoro Ongala ambaye alikuwa mwanamuziki gwiji nchini na mama yake Muingereza alikuwa ni mwalimu.

Kisoka alianzia katika timu ya Abajalo na kisha akazichezea, Yanga, Kajumulo, Vasby United, Umea, Azam FC na Sundsvall.

Baada ya uongozi wa KMC kuvunja mkataba na Kally Ongala, jukumu la kusimamia benchi la ufundi la timu hiyo katika mechi nne ilizobakiza za Ligi Kuu imeliacha kwa kocha wa viungo, Adam Mbwana.

Kocha wa Viungo wa KMC, Adam Mbwana. Picha na Charles Abel.

Mechi nne ambazo KMC imebakiza ni dhidi ya Simba, Tabora United, Pamba Jiji FC na Mashujaa FC.