Juventus yamvuta Luiz, yamwania Santiago


Muktasari:

  • Juventus imeingia tena vitani na Chelsea kwa ajili ya kumwania  beki wa Nottingham Forest, Murillo Santiago.

Turin, Italia. Klabu ya Juventus imekamilisha usajili wa staa wa Aston Villa Douglas Luiz kwa kitita cha pauni 45 milioni huku akiwa Italia anasubiri kufanya vipimo vya afya.

Juventus imekamilisha dili hilo ikiwa imefanikiwa kuwashinda Arsenal na Chelsea ambazo zilikuwa zinamwania staa huyo ambaye msimu uliopita alifanikiwa kufanya mambo makubwa kwenye Ligi Kuu England.

Pia Juventus imeingia tena vitani na Chelsea kwa ajili ya kumwania  beki wa Nottingham Forest, Murillo Santiago.

Chelsea ilipeleka ofa kuhakikisha inampata Murillo, ambaye klabu yake imesema kuwa ipo tayari kumuuza endapo tu itafanikiwa kupata kiwango sahihi cha fedha sokoni huku bei yake ikitajwa kuwa pauni 70 milioni.

Staa huyo alifanikiwa kuichezea Forest michezo 36 msimu uliopita na kuzivutia klabu kadhaa kwenye ligi kubwa barani Ulaya.

Kwa mujibu wa taarifa, Luiz anatarajiwa kutambulishwa nchini Italia siku chache zijazo akiwa ameshaanga kwenye timu yake ya Villa ambayo kwa misimu mitano aliitumikia kwenye michezo 204 na kuifungia mabao 22.

Arsenal ilikuwa inapewa nafasi kubwa ya kumpata mchezaji huyo lakini dau kubwa la usajili likazuia dili hilo.