Mastaa 36 warahisisha soko usajili Ulaya

Mchezaji Kylian Mbappe

Berlin,Ujerumani. Wakati dirisha la uhamisho la majira ya kiangazi likitarajiwa kufunguliwa keshokutwa barani Ulaya, uwepo wa nyota 36 wanaomaliza mikataba katika timu mbalimbali unazipa uhakika baadhi ya klabu kutotumia bajeti kubwa ya fedha kuwanasa tofauti na iwapo wangekuwa na mikataba na timu zao.

Pengine klabu zao za sasa zingehitaji kiasi fulani cha fedha katika kuwafungulia milango wachezaji hao kujiunga na klabu nyingine lakini imekuwa tofauti na sasa ambapo timu zinazowamiliki wachezaji hao hazitopata chochote kutokana na nyota hao kuwa huru.

Na katika kundi la mastaa hao 36, wapo ambao inaripotiwa tayari wameshasaini mikataba ya kujiunga na klabu nyingine ingawa pia wapo wale ambao hadi sasa haijajulikana kama watabakia katika timu walizopo au wataondoka.

Katika orodha ya mastaa hao 36, jina la Kylian Mbappe ndio linaonekana kutikisa zaidi baada ya nyota huyo kugomea mkataba mpya wa kuitumikia PSG licha ya ofa nono ya fedha ambayo alitengewa na anatajwa kwamba atajiunga na Real Madrid kwa uhamisho huru akihitimisha miaka nane na nusu ya kuitumikia ligi ya Ufaransa.

Mbappe mwenye umri wa miaka 25, anaondoka PSG akiwa ameifungia idadi ya mabao 250 katika michezo 308 huku akipiga pasi za mwisho 108.

Kiungo wa ulinzi wa Juventus, Adrien Rabiot (29) ni nyota mwingine ambaye yuko huru baada ya mkataba wake na timu hiyo ya Italia aliyoitumikia kwa miaka mitano kufikia tamati.

Klabu mbalimbali zinatajwa kumuwania nyota huyo wa zamani wa PSG na miongoni mwa hizo ni Manchester United ambayo inataka kumsajili kwa ajili ya kuziba pengo la Casemiro ambaye amefunguliwa milango ya kutokea.

Nahodha na mkongwe wa Croatia, Luka Modric (38) atakuwa sokoni katika kipindi hiki baada ya mkataba wake na Real Madrid aliyoitumikia kwa miaka 12 tangu alipojiunga nayo mwaka 2012 kutokea Tottenham Hotspur.


Modric anaondoka Real Madrid kwa heshima kubwa akiwa ameichezea mechi 533 na kuhusika na mabao 125 ambayo 39 amefunga na 86 alitoa pasi za mwisho na ameshinda idadi ya mataji 25 akiwa na timu hiyo na yanaweza kufikia 26 ikiwa itaibuka na ushindi katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Borussia Dortmund, Jumamosi, Juni Mosi.

Kwa timu inayosaka beki wa kati, inaweza kutotumia gharama kubwa kwa kumnyakua nyota wa Ufaransa, Raphaël Varane ambaye baada ya mkataba wake wa kuitumikia Manchester United kwa miaka mitatu kumalizika, timu hiyo imeamua kutomuongezea mkataba mpya.

Licha ya mategemeo makubwa ambayo Manchester United ilikuwa nayo kwa mchezaji huyo wakati inamsajili mwaka 2021, mambo yalienda tofauti kutokana na Varane kukabiliwa na majeraha ya mara kwa mara lakini pia akishindwa kuonyesha kiwango bora uwanjani.

Fenerbahce ya Uturuki inaonekana imeshindwa majaribio yake kadhaa ya kumbakisha mshambuliaji Michy Batshuayi na sasa nyota huyo ataipa mkono wa kwaheri timu hiyo ya Uturuki ambayo ameichezea tangu 2022.

Katika msimu uliomalizika, Batshuayi ambaye ni raia wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 30, ameifungia Fenerbahce, mabao 12 katika mechi 27.

Mkataba wa nyota wa Monaco, Wissam Ben Yeder aliyefunga mabao 16 katika Ligi Kuu ya Ufaransa msimu ulimalizika, nao umefikia tamati na mshambuliaji huyo mwenye umri wa 33 ataondoka klabuni hapo baada ya kucheza kwa misimu mitano mfululizo.

Anthony Martial naye hatokuwa sehemu ya kikosi cha Manchester United msimu ujao baada ya kuaga rasmi kufuatia kumalizika kwa mkataba wake na timu hiyo aliyochezea kwa miaka tisa.

Katika kipindi chote ambacho Martial ameichezea Manchester United, ameifungia mabao 90 katika mechi 317 huku akipiga pasi za mwisho 47.

Thiago Alcantara wa Liverpool naye ataondoka kama mchezaji huru katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi baada ya mkataba wake na timu hiyo kumalizika.


Idadi ya mabao matatu tu ndio yaliyofungwa na Thiago katika mechi 98 alizoichezea huku akiwa amepiga pasi sita tu za usaidizi wa manao mengine.

Kiwango kisichoridhisha cha Nicolas Pepe kimeifanya timu yake Trabzonspor kutomuongezea mkataba baada ya ule wa sasa wa mwaka mmoja kumalizika na hivyo mshambuliaji huyo wa Ivory Coast ana kibarua cha kusaka timu mpya.

Pepe amefunga mabao sita na kupiga pasi za mwisho tatu katika mechi 23 alizoichezea Trabzonspor.

Liverpool pia haitokuwa na beki wake Joel Matip baada ya nyota huyo wa Cameroon kumaliza mkataba wake na hatoongezewa mpya kama ilivyo kwa mshambuliaji Luka Jovic ambaye amemaliza mkataba wa kuitumikia AC Milan.

Wachezaji wengine ambao mikataba yao imemalizika na watakuwa huru katika dirisha la usajili la kiangazi ni Wilfred Ndidi na Kelechio Iheanacho (Leicester City), Christian Kouame na Gaetano Castrovilli (Fiorentina), Mario Hermoso (Atletico Madrid), Guido Rodriguez na Juan Miranda (Real Betis), Lloyd Kelly (Bournemouth), Rafa (Benfica) na Daichi Kamada (Lazio).

Kuna Che Adams (Southampton), Alex Berenguer (Athletic Bilbao), Ryan Sessegnon (Tottenham Hotspur), Yusuf Yazici (Lille), Andre Gomes (Everton), Bertrand Traore (Villarreal), Ben Johnson (West Ham), Vladimir Coufal (West Ham), Mady Camara (Olympiacos), Chris Wood (Nottingham Forest) na John Lundstram (Rangers).