Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jaji Warioba ataka Simba, Yanga zikutane fainali

Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba akizungumza na waandishi wa habari wa Mwananchi

Muktasari:

  • Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema anaamini Simba na Yanga zina uwezo wa kushinda kwenye mechi za marudiano za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, leo usiku timu hizo zitakapocheza ugenini.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema anaamini Simba na Yanga zina uwezo wa kushinda kwenye mechi za marudiano za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, leo usiku timu hizo zitakapocheza ugenini.

Jaji Warioba amekwenda mbali zaidi na kueleza kwamba, matamanio yake kwa timu hizo za Tanzania ni kuona zinafanya vizuri kwenye robo fainali leo,  kisha nusu na hatimaye zitinge fainali na kucheza zenyewe kwa zenyewe fainali hiyo.

Timu hizo zipo ugenini, mechi za leo zikiwa za kuamua hatma yao kama zitafuzu nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika au la.

Simba inarudiana na Al Ahly kwenye Uwanja wa Cairo International nchini Misri kuanzia saa 5:00 usiku, inahitaji ushindi wa kuanzia mabao mawili ili itinge nusu fainali baada ya kufungwa nyumbani bao 1-0 jijini Dar es Salaam wiki iliyopita.

Yanga yenyewe itacheza Uwanja wa Loftus Jijini Pretoria Afrika Kusini kuanzia saa 3:00 usiku.

Nayo inahitaji ushindi wowote au sare ya mabao dhidi ya Mamelodi Sundowns ili ifuzu nusu fainali baada ya kutoka suluhu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Aprili 5, 2024 ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Jaji Warioba amesema timu hizo za Tanzania zina nafasi ya kushinda ugenini.

"Nilishangaa kwanini Yanga haikushinda mechi iliyopita, hata Simba pia, zilicheza vizuri hapa nyumbani.

"Kama zikicheza vile zilivyocheza, uwezo wa kushinda upo, mimi natamani, zifanye vizuri ili zije zikutane zenyewe kwa zenyewe kwenye fainali,".

Amesema, kama zitafanikiwa zikutane fainali, kwake yoyote kati ya timu hizo kongwe za soka nchini zenye utani wa jadi anapenda ishinde.

"Hata nyumbani kwangu, tukiwa tunaangalia mpira, kwenye timu hizi,  mimi huwa nasifia mchezaji anayefanya vizuri, nikifanya hivyo, pale kwangu kuna wale wa Simba na Yanga utawaona wanasema sema, lakini mimi huwa naangalia inayofanya vizuri.

"Kwenye Ligi ya Mabingwa natamani zote zifanye vizuri, zifike hadi fainali ili zikutane zenyewe kwa zenyewe, ikitokea hivyo zikacheza fainali, basi yoyote itakayoshinda kwangu ni sawa, ila natamani zipambane zifanye vizuri zikutane kwenye fainali," amesema.

Kama zitashinda mechi za leo, Simba itacheza nusu fainali na mshindi wa jumla katí ya TP Mazembe au Petro de Luanda ya Angola wakati Yanga itacheza na mshindi wa jumla katí ya Esperance ya Tunisia au ASEC Mimosas ya Ivory Coast kwenye nusu fainali.

Katika hatua nyingine, Jaji Warioba amezungumzia tofauti ya ufuatiliaji michezo zamani na sasa.

Amesema, enzi zao walikuwa wakizifahamu zaidi timu za ndani kuliko za nje.

"Tulikuwa tunafuatilia soka, riadha na kuzijua timu na wachezaji, hivi sasa watu wanafuatilia zaidi timu za nje, wanazijua hizo zaidi ya zile za ndani,".