Isak aanza kunukia Anfield

Muktasari:
- Liverpool ipo kwenye mchakato wa kunasa mastaa wa maana ili kumpa Kocha Arne Slot kikosi chenye nguvu kubwa ya kushindana kwenye kusaka mataji msimu ujao.
Liverpool, England. Liverpool itapenda kuendelea kufungua pochi dirisha hili la majira ya kiangazi huku mpango wao ni kunasa huduma ya straika Alexander Isak lakini dili hilo litawaingiza kwenye matatizo makubwa.
Liverpool ipo kwenye mchakato wa kunasa mastaa wa maana ili kumpa Kocha Arne Slot kikosi chenye nguvu kubwa ya kushindana kwenye kusaka mataji msimu ujao.
Jeremie Frimpong alishanaswa na miamba hiyo ya Anfield akitokea Bayer Leverkusen kama mbadala wa Trent Alexander-Arnold, aliyetimkia Real Madrid. Liverpool imewanasa pia Florian Wirtz na Milos Kerkez kwa ada ya Pauni 116.5 milioni na Pauni 40 milioni kutoka Leverkusen na Bournemouth mtawalia.
Na Liverpool huenda haijamaliza kusajili kwa nyota hao, ambapo sasa ipo kwenye mchakato wa kumfukuzia beki wa kati wa Crystal Palace, Marc Guehi akitazamwa kama mbadala wa Jarell Quansah.
Straika wa Newcastle United, Isak ni jina jingine linalohusishwa na Liverpool na mkali huyo wa Sweden ni moja ya wachezaji ambao miamba hiyo ya Anfield ikapenda kuwa na huduma yake.
Lakini, kihesabu Liverpool inaonekana kutokuwa na nafasi ya kumsajili Isak kwenye dirisha hili. Newcastle itahitaji ilipwe zaidi ya Pauni 150 milioni kwa ajili ya mshambuliaji huyo katika dirisha hili, ada ambayo itakuwa mlima mzito kwa Liverpool kupanda kutokana na pesa ilizotumia hadi sasa.
Hadi sasa hakuna dili rasmi lililozungumzwa baina ya Liverpool na Newcastle kuhusu Isak - ambaye anaonekana kufurahia maisha yake ya sasa huko St James’ Park.
Hata hivyo, kocha wa Newcastle, Eddie Howe alizungumzia juu ya hatima ya Isak na hakufuta uwezekano wa kumpiga bei straika huyo - lakini aliwaambia mabosi wake atapenda sana kama mchezaji huyo atabaki.
Alisema: “Kamwe sitatoa uhakika wa juu ya hilo kwa kila mchezaji na hilo pia silisemi kwenye hatima ya Alex.”