Isak aanza kuhesabu siku Newcastle apiga hesabu za Anfield
Muktasari:
- Kwa sasa, macho yote yatakuwa kwa Isak ataendelea kusalia Newcastle au atasafiri kwenda Anfield? Muda ndio utakaotoa jibu.
Mshambuliaji wa Newcastle United, Alexander Isak, ameingia tena kwenye vichwa vya habari baada ya kuonekana akifanya mazoezi peke yake huku mazungumzo kuhusu mustakabali wake yakizidi kushika kasi.
Isak, ambaye kwa sasa analipwa pauni 120,000 (Sh420 milioni) kwa wiki, ameripotiwa kudai mkataba mpya wenye mshahara wa pauni 300,000 (Sh1 bilioni) kwa wiki ili aendelee kubaki St. James’ Park kiwango ambacho kitavunja kabisa muundo wa malipo ndani ya klabu hiyo inayomilikiwa na Waarabu wa Saudi Arabia.
Licha ya Newcastle kusisitiza kuwa haitaki kumuuza mchezaji huyo, tetesi za kutakiwa na mabingwa wa England, Liverpool, zimeendelea kushika kasi. Inaripotiwa kuwa Liverpool huenda wakalazimika kutoa zaidi ya pauni milioni 125 (Sh437 bilioni) ili kumnasa straika huyo raia wa Sweden aliyejiunga na Newcastle mwaka 2022 akitokea Real Sociedad kwa dau la pauni milioni 60.
Katika picha iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii, Isak ameonekana akifanya mazoezi kivyake akiwa na mmoja wa wafanyakazi wa Newcastle, jambo lililotafsiriwa na mashabiki kuwa ni ishara ya kujiandaa kuondoka.
Meneja wa Newcastle, Eddie Howe, amethibitisha kuwa aliamua kumtoa Isak katika kikosi kilichochapwa 4-0 na Celtic kwenye mechi ya kirafiki siku ya Jumamosi kwa sababu ya tetesi zinazoendelea kumuhusu.
"Nilichagua kumrudisha nyumbani. Hatukutaka akae jukwaani bila kucheza halafu akawa kwenye mazingira ya mashinikizo ya tetesi hizo. Tulikubaliana kuwa ni bora asiwepo uwanjani. Alikuwa sawa kiafya na amekuwa akifanya mazoezi vizuri," amesema Howe.
Ingawa Howe alikiri kuwa hakuna uhakika wa asilimia 100 kuhusu mustakabali wa mchezaji yeyote, alisisitiza kuwa Isak ana furaha Newcastle na hajawahi kuonesha dalili za kutaka kuondoka.
"Isak ni mmoja wa wachezaji wetu wasio na mbadala. Ni vigumu sana kuwapata wachezaji wa aina yake, hivyo tunapaswa kuwathamini sana. Tumekuwa tukizungumza naye, na kwa kweli hajaleta matatizo yoyote," amesema kocha huyo.
Newcastle wanatarajia kuanza ziara yao ya maandalizi ya msimu mpya wiki hii, huku wakikabiliwa na Arsenal jijini Singapore Julai 27, kabla ya kuvaana na kikosi cha nyota wa Ligi Kuu ya Korea Kusini (K League All-Stars) na Tottenham nchini Korea Kusini.
Kwa hali ilivyo sasa, macho yote yatakuwa kwa Isak ataendelea kusalia Newcastle au atasafiri kwenda Anfield? Muda ndio utakaotoa jibu.