Liverpool kumchomoa Isak Newcastle
Muktasari:
- Kwa hesabu rahisi, uuzwaji wa Nunez na Diaz unaweza kufadhili sehemu kubwa ya gharama ya kumleta Isak Anfield msimu ujao.
Klabu ya Liverpool imewasilisha nia ya kumsajili mshambuliaji wa Newcastle United, Alexander Isak, kwa dau la pauni milioni 120 zaidi ya shilingi trilioni 4 za Kitanzania, kwa mujibu wa taarifa kutoka The Athletic.
Ingawa bado hawajatoa ofa rasmi, Liverpool wameripotiwa kuwa wanafahamu msimamo wa Newcastle kwamba mshambuliaji huyo wa Sweden hauzwi. Hata hivyo, wanabaki na matumaini kuwa dili linaweza kufanikishwa.
Isak, mwenye umri wa miaka 25, alifunga mabao 23 kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita, akizidiwa na Mohamed Salah wa Liverpool aliyefunga mabao 29. Kwa jumla, Isak amefunga mabao 62 katika mechi 109 tangu kujiunga na Newcastle kutoka Real Sociedad kwa ada ya pauni milioni 60 mwaka 2022.
Tayari Isak amewasaidia Newcastle kutwaa Kombe la Carabao mwezi Machi, taji lao la kwanza kubwa ndani ya miaka 70.
Liverpool watafuta mbadala
Iwapo dili la Isak litagonga mwamba, Liverpool wameweka macho yao kwa Hugo Ekitike wa Eintracht Frankfurt kama mpango mbadala. Cha kushangaza ni kwamba Newcastle nao wanamtaka mfaransa huyo, na tayari ofayao ya pauni milioni 70 imekataliwa.
Liverpool wanashusha mzigo
Liverpool tayari wametumia pauni milioni 185 kwa kusajili wachezaji wapya wanne akiwemo Florian Wirtz, aliyesajiliwa kutoka Bayer Leverkusen kwa kuvunja rekodi ya usajili Uingereza.
Wakati huo huo, Liverpool wapo kwenye mazungumzo ya kuachana na mshambuliaji wao Darwin Nunez, ambaye ameonekana kutovutia sana chini ya kocha mpya Arne Slot. Klabu ya Napoli na Al-Hilal ya Saudi Arabia zimeonyesha nia, lakini Liverpool wanataka pauni milioni 70.
Luis Diaz asumbuliwa na Bayern Munich
Katika hatua nyingine, Liverpool walikataa ofay a pauni milioni 58.6 kutoka Bayern Munich kwa winga wao wa Colombia, Luis Diaz. Klabu hiyo ya Merseyside imeweka thamani ya pauni milioni 86 kwa mchezaji huyo mwenye mkataba hadi 2027, ingawa wamesema hawana mpango wa kumuuza msimu huu.
Kwa hesabu rahisi, uuzwaji wa Nunez na Diaz unaweza kufadhili sehemu kubwa ya gharama ya kumleta Isak Anfield msimu huu.