Injinia Mkenya apewa Dabi ya Kariakoo Muungano
Mwamuzi Dickes Mimisa kutoka Kenya ambaye atachezesha mchezo wa fainali ya Kombe la Muungano utakaowakutanisha watani wa jadi, Yanga na Simba, Aprili 29, 2026 kwenye Uwanja wa Amaan Complex, Zanzibar
Muktasari:
- Simba na Yanga zitashuka dimbani kuanzia saa 2:15 usiku leo Jumatano kusaka taji la kwanza msimu huu kwa kila mmoja.
Zanzibar. Kamati ya Mashindano ya Muungano imepindua meza, baada ya kufuata mwamuzi Kenya wa kuamua mchezo wa Fainali kati ya Yanga dhidi ya Simba.
Mpaka Jumanne Aprili 28, 2026 jioni kamati hiyo ilikuwa haijamtangaza mwamuzi wa mchezo huo utakaopigwa leo saa 2:15 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar.
Kamati hiyo ikishirikiana na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) limemtangaza Dickes Mimisa kuwa mwamuzi wa mchezo huo.
Mimisa raia wa Kenya kitaaluma ni injinia wa ujenzi mkazi wa Jiji la Mombasa nchini Kenya ndiye atasimamia mchezo huo.
Mimisa atasaidiwa na Ally Mbwana atakayekuwa msaidizi wa kwanza, wakati Yusuf Shombe akiwa msaidizi wa pili, wote wakiwa wanatoka Zanzibar na Isihaka Mwalile akiwa mwamuzi wa nne mezani kutoka Tanzania Bara huku Ramadhan Kibo akiwa kamishna wa mechi.
Mimisa amewahi pia kuwa mwamuzi kwenye mashindano mbalimbali Afrika yakiwemo Afcon U17 (2023), Afcon U20 (2024), CHAN (2025) na AFCON (2025).
Wakati huohuo taarifa hiyo imefanya mabadiliko ambapo mgeni rasmi kwenye mchezo huo atakuwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.
Awali kamati hiyo ilimtangaza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi kuwa angekuwa mgeni rasmi kabla ya mabadiliko hayo.