Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hizi hapa hesabu mpya kuelekea Kariakoo Dabi

Muktasari:

  • Yanga itakutana na Simba kwenye fainali ya Kombe la Muungano itakayopigwa Aprili 29 mwaka huu kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar kisha timu hizo zitakutana tena kwenye mechi ya Ligi Kuu itakayochezwa Mei 3, 2026 jijini Dar es Salaam.

Unguja. Kuna hesabu mpya za Kocha wa Simba, Steve Barker na yule wa Yanga, Pedro Goncalves kuelekea mechi mbili za Dabi ya Kariakoo zitakazochezwa ndani ya takribani siku nne. Ikianzia Zanzibar, kisha kumaliziwa Dar es Salaam.

Hiyo inatokana na Simba na Yanga kufuzu fainali ya Kombe la Muungano itakayochezwa kesho Jumatano ya Aprili 29 mwaka huu, huku pia awali kukiwa na ratiba ya Ligi Kuu Bara iliyopangwa kufanyika Mei 3, 2026.

Simba ambayo ilikata tiketi ya kwenda fainali juzi Jumapili baada ya kuichapa Mlandege kwa mabao 3-0, kocha wake Steve Barker alisema amelazimika kubadili hesabu zake baada ya kufikiria namna ya kuingia kwenye dabi hizo mbili.

Winga wa Simba, Elie Mpanzu wakati akijaribu kumpita beki wa Yanga, Dickson Job katika mechi ya Ngao ya Jamii iliyopigwa Septemba 16, 2026

Barker alisema Simba inalitaka Kombe la Muungano kutokana na ukame wa mataji ndani ya klabu hiyo ambapo kikosi chake kitaingia na akili kubwa kuhakikisha wanatoka salama kwenye fainali hiyo.

Kocha huyo alisema hautakuwa mchezo rahisi kwa timu zote lakini akachekelea kwamba kila mchezaji wake muhimu yuko tayari kwa mechi hiyo kubwa ya uamuzi ambayo inasubiriwa na mashabiki wa Simba kuona kombe linatua Msimbazi.

"Unajua kwamba Simba haijashinda taji ndani ya misimu minne, kwahiyo kuna akili mpya hapa lazima tuizingatie kuhakikisha kwamba tunafanya vizuri kwenye hii fainali ili mashabiki wetu wasiumie," alisema Barker.

"Haitakuwa mechi rahisi, tunakwenda kukutana na bingwa mtetezi, unapotaka kuwa bora lazima ushindane na walio bora, kitu kizuri ni kwamba wachezai wetu wako salama, ni hatua ya kwenda kufanyia kazi mbinu kabla ya mchezo huo."

Simba imekuwa ikisaka mafanikio ya kubeba makombe kwa muda mrefu, huku ikifanikiwa kubeba Kombe la Muungano 2024 ilipoifunga Azam. Kabla ya hapo, mara ya mwisho ilishinda Ngao ya Jamii 2023.

Wakati Barker akiyasema hayo, Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves amesema kikosi chake kina hesabu za kwenda kulinda heshima yao kwa kutetea ubingwa wanaoushikilia lakini pia rekodi ya kutopoteza mbele ya wekundu hao kwa muda mrefu.

Pedro amesema kikosi chake kimeimarika na kwamba sasa wanacheza kama timu bingwa inayotaka kwenda kutetea mafanikio hayo ambapo watajiandaa kwenye kila kitu ili washinde mechi hiyo.

"Timu hizi mbili zinatoka kukimbizana kwenye ligi ni lazima tuiheshimu Simba sio mchezo rahisi na itakuwa fainali ngumu, lakini kwetu sisi tulijiandaa kukutana na timu yoyote, tuna jukumu la kutakiwa kulinda ubingwa wetu lakini pia rekodi yetu," alisema Pedro.

"Hakuna nafasi ya kuhofia lolote, tunakwenda kujipanga kukabiliana nao, tuna wachezaji bora wanaotaka kuthibitisha thamani na ubora wao, hii ni timu ambayo ina kiu ya mafanikio makubwa."

Yanga itakutana na Simba kwenye fainali ya Kombe la Muungano itakayopigwa Aprili 29 mwaka huu kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar ambapo ikimalizika hiyo timu hizo zitakwenda kukutana kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa Mei 3, 2026 jijini Dar es Salaam.

Rekodi zinaonyesha tangu mara ya mwisho Simba iifunge Yanga katika Ngao ya Jamii Agosti 13, 2023 kwa penalti 3-1, imepoteza mechi sita mfululizo walizokutana huku ya mwisho ikimalizika kwa 0-0.

Wakati huohuo, mshambuliaji wa Simba, Seleman Mwalimu, amemtumia salamu Prince Dube wa Yanga akimwambia anakitaka kiatu cha dhahabu ambayo ni tuzo maalum kwa mfungaji bora wa mashindano.

Mwalimu na Dube wana jambo lao msimu huu ambapo kule kwenye Ligi Kuu Bara, Dube anaongoza kwa kufunga mabao nane sawa na Fabrice Ngoy wa Namungo, huku Mwalimu akifunga sita akiwa kinara ndani ya Simba.

Pia Dube anaongoza kwa ufungaji kwenye Kombe la Muungano akiwa na mabao matatu, akifuatiwa na Mwalimu aliyefunga mawili na wote wawili watashuka dimbani Jumatano hii kuzipambania Yanga na Simba kwenye mchezo wa fainali wa michuano hiyo utakaothibitisha nani atamaliza kinara.

Mwalimu amesema anaitaka tuzo ya ufungaji bora akianzia kwenye mashindano ya Muungano na kwa namna Simba inavyocheza anaamini ataweza kufanya kweli.

Mshambuliaji huyo amesema ubora wa timu hiyo ndio umempa wepesi wa kuzidisha kasi ya kufunga akifurahia kucheza na viungo wabunifu ambao wamekuwa wakimtengenezea pasi nyingi.

Beki wa kushoto wa Simba, Nickson Kibabage wakati akijaribu kumzuia kiungo mshambuliaji wa Yanga, Max Nzegeli katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan Complex, Machi Mosi mwaka huu.

"Kweli naitaka tuzo ya ufungaji bora, kila mshambuliaji ana ndoto hiyo ya kuwa mfungaji bora na mimi nitaanzia hapa kwenye Muungano, najua kuna mtu yupo juu yangu lakini nitapambana kutafuta mabao kwenye mchezo wa fainali," alisema Mwalimu.

"Kitu ninachofurahia ni kucheza kwenye timu yenye viungo wengi wabunifu, kila mshambuliaji angependa kucheza kwenye kikosi cha namna hii, nimekuwa nafunga ni kutokana na ubora wa viungo wa timu yetu."

Aidha Mwalimu aliongeza kuwa katika kiu yake hiyo anatamani itimie ili aweze kuwabeba kwa heshima wachezaji wazawa katika kuichukua tuzo hiyo kutokana na wageni wengi kutawala eneo hilo.

"Ninapoipigania tuzo hii nawafikiria pia wachezaji wenzangu wazawa, unajua wenzetu wa kigeni wamekuwa wanachukua sana mafanikio haya lakini kwangu nataka iwe zamu ya sisi wazawa pia."