Hoteli ya England gumzo, wakianza maandalizi Kombe la Dunia
Muktasari:
- Katika Fainali za Kombe la Dunia 2026, England imepangwa katika kundi L na timu za Croatia, New Zealand na Costa Rica.
Kikosi cha wachezaji 26 wa England tayari kipo Marekani kwa ajili ya kufanya maandalizi ya mwisho ya Fainali za Kombe la Dunia zitakazochezwa kuanzia Juni 11 hadi Julai 19 mwaka huu.
Msafara wa England umefikia katika jiji la Florida ambako itakaa kwa muda wa siku 12 kabla ya kuhamia katika kambi ambayo itapangiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).
Ikiwa hapo Florida, England imefikia katika Hoteli ya kifahari ya Belgrove Resort iliyopo katika eneo la West Palm Beach, Florida.
Hoteli hiyo inamilikiwa na bilionea Steve Witkoff ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais wa Marekani, Donald Trump.
Muonekano wa madhari ya nje ya Hotel ilipofikia timu ya Taifa ya England, Florida, Marekani kwa ajili ya maandalizi ya Fainali za Kombe la Dunia 2026. Picha na Mtandao
Witkoff ndiye alikuwa akicheza gofu na Trump wakati wa jaribio la kupigwa risasi lililowahi kumkuta Rais huyo wa Marekani mwaka jana.
Ni miongoni mwa hoteli zilizojengwa kwa gharama kubwa nchi Marekani ambapo ujenzi wake umegharimu kiasi cha Dola 100 milioni (Sh261 bilioni).
Ndani ya hoteli hiyo, kuna mabwawa makubwa matatu ya kisasa ya kuogelea, ukumbi wa huduma ya SPA na kiwanja cha kuchezea gofu.
Muonekano wa Hotel ilipofikia timu ya Taifa ya England, Florida, Marekani kwa ajili ya maandalizi ya Fainali za Kombe la Dunia 2026. Picha na Mtandao
Pia kuna viwanja vinne tofauti vya kisasa vya mchezo wa tenisi, viwanja viwili vya mchezo wa Pickleball na pia kuna ukumbi maalum wa kumsaidia mtu kupata utulivu baada ya kukutana na kelele.
Gharama ya chini ya chumba kimoja katika hoteli hiyo ni Dola 265 (Sh690,324) na gharama ya chumba cha kifahari kwa usiku mmoja ni Dola 959 (Sh2.5 milioni).
Baada ya siku 12 za kuwa hapo, England itaelekea Kansas City ambako ndiko itakuwepo huko katika kipindi chote cha mashindano.
Juni 17, England itacheza na Croatia na Juni 23 itakabiliana na Ghana na itamalizia hatua ya makundi kwa kucheza na Panama Juni 28.