Hili ndiyo kombe jipya inaloliwania Simba

Muktasari:
- Timu ya Simba inapambana kuhakikisha kuwa inatwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii.
Baada ya kuzindua kombe jipya la Ligi ya Mabingwa Afrika Alhamisi iliyopita, Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) leo Jumapili limezindua kombe jipya la Shirikisho, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya fainali ya mashindano hayo itakayopigwa saa chache zijazo.

Kombe hilo jipya kwa mashindano ya klabu barani Afrika limebuniwa upya kwa muundo wa kuvutia unaoakisi historia tajiri ya mashindano hayo maarufu Afrika.
Uundaji wa kombe hili ni sehemu ya mkakati mpana wa CAF wa kuboresha na kupandisha hadhi ya mashindano yake. Lengo ni kuongeza mvuto wa mashindano ya soka la Afrika kwa macho ya dunia.
Kombe hilo linawakilisha matumaini, mshikamano na ubora katika soka la bara hili. Juu ya kombe hilo kuna mpira wa dhahabu iliyopigwa ‘matte’, ukionesha ramani ya Afrika kwa dhahabu inayong’aa, ikiwa ni ishara ya fahari ya bara.
Mikono miwili ya dhahabu iliyopigwa ‘matte’ inauinua mpira huo juu, kama ishara ya mshikamano na nguvu.
Mwili wa kombe huo umetengenezwa kwa fedha inayong’aa, ukiwa na alama ya radi ya dhahabu inayoashiria kasi, ushindani na hamasa ya mashindano.
Msingi wa kombe umetengenezwa kwa marumaru, ikiwa ni ishara ya jadi na heshima, na umechorwa jina la mashindano pamoja na washindi wa zamani.
Kombe hilo lina urefu wa sentimita 45 na uzito wa kilo 8 hadi 10, likiwa limeundwa mahususi kuonyesha heshima ya ubingwa na kuakisi ari ya ushindani ya soka la Afrika.
Timu ya Simba inapambana kuhakikisha kuwa inatwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii.
RS Berkane inaingia kwenye mechi hiyo ikiwa mbele kwa mabao 2-0 baada ya ushindi iliyoupata katika mechi ya kwanza iliofanyika Morocco.