Gyokeres asusia mazoezi Sporting kisa Arsenal
Lisbon, Ureno. Mvutano mkubwa umeibuka kati ya klabu ya Sporting na mshambuliaji wake, Viktor Gyokeres, ambaye amesusia mazoezi ya maandalizi ya msimu mpya huku akihusishwa na uhamisho kwenda Arsenal.
Rais wa klabu hiyo, Frederico Varandas, amethibitisha kuwa nyota huyo raia wa Sweden atachukuliwa hatua za kinidhamu baada ya kutotokea kambini licha ya kuongezewa mapumziko hadi Julai 12.
“Uvumilivu wetu umefikia mwisho. Tutampa faini kubwa na atatakiwa kuomba msamaha kwa wenzake kambini,” amesema Varandas alipokuwa akizungumza na shirika la habari la Lusa.
Inadaiwa kuwa Gyokeres tayari amekubali masharti binafsi na Arsenal, huku dau la uhamisho likiwa ndio kikwazo pekee. Hata hivyo, klabu hiyo ya London haijakubali kulipa kitita cha pauni milioni 70 (Sh222 bilioni) kinachodaiwa na Sporting.
Varandas ameweka wazi kuwa hawako tayari kulegeza msimamo wao:
“Kama kuna watu wanafikiri kususia kwake kutatufanya turahisishe mchakato wa kumuuza, basi wamekosea sana. Hali hiyo inazidi kumuweka pabaya mchezaji. Hakuna mtu aliye juu ya maslahi ya klabu.”
Gyokeres aliyejiunga na Sporting kwa dau la pauni milioni 20 kutoka Coventry City mwaka 2023, amekuwa moto wa kuotea mbali kwa kufunga mabao 97 katika mechi 102 alizocheza katika mashindano yote.
Msimu uliopita pekee, alitikisa nyavu mara 54 na kuwafanya mashabiki wa klabu hiyo kumpa heshima kama mmoja wa washambuliaji hatari zaidi barani Ulaya.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, mshambuliaji huyo amekuwa akitamani kurejea England ili kupata fursa ya kuonesha uwezo wake kwenye EPL, baada ya kushindwa kupata nafasi alipokuwa Brighton.
“England ni moja ya ligi kubwa Ulaya. Nilikaa huko kwa miaka kadhaa bila hata kuchezeshwa mechi moja. Kwa hiyo, ni jambo ninalotamani kulifanikisha ni kama kisasi,” amesema Gyokeres katika mahojiano ya nyuma.
Kwa sasa, Arsenal chini ya kocha Mikel Arteta inahaha kusaka mshambuliaji mpya kabla ya kikosi chake kusafiri kwenda Singapore Julai 19 kwa ajili ya ziara ya maandalizi ya msimu mpya.
Lakini kutokana na msimamo wa Sporting, inaonekana wazi kuwa Arsenal watalazimika kuongeza dau lao ili wamnase mshambuliaji huyo.